………….
Na Sixmund Begashe, Same
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeeleza kuridhishwa na uwekezeji uliofanywa na Serikali katika mradi wa Faru ambao umesaidia kuchechemua ongezeko la watalii katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi iliyopo Wilayani same Mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, mara baada ya kutembelea na kukagua mradi huo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb), amesema Mradi huo ni wakujivunia kwa kuwa umeonesha matokeo chanya kwa kuongeza kwa haraka idadi ya watalii na mapato katika hifadhi hiyo.
Mhe. Masanja amebainisha kuwa, mafanikio ya mradi huo ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuongeza mazao mapya ya utalii, kuongeza idadi ya siku za wageni kutalii nchini na kuinua sekta za Maliasili na Utalii
Aidha Mhe. Masanja ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri ya usimamizi wa mradi huo,na kuwapongeza askari kwa uzalendo na ujasiri katika kuwalinda Faru hao ambao walikuwa hatarini kutoweka.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameishukuru Kamati hiyo kwa ziara waliyoifanya hifadhini hapo kukagua na kujionea mradi huo na kwamba Wizara itafanyia kazi kwa haraka maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.
Akieleza madhumuni ya mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amesema ni pamoja na kuongeza uhifadhi zaidi wa mnyama Faru ambaye alikuwa hatarini kutoweka, kuvutia zaidi watalii katika hifadhi hiyo, kutengeneza ajira hususani kwa vijana na kuchangia zaidi katika pato la Taifa.
Dkt. Abbasi ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo hapa nchini ili kufurahi urithi adhimu wa Maliasili









