Mawakili wapinga uhalali wa Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Oktoba 29- 2

Dar es Salaam. Katika mwendelezo wa mapitio ya uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ya shauri la kupinga Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Oktoba 29, 2025, baada ya kuangalia msingi wa madai ya waombaji, sasa tunaangalia majibu ya wajibu maombi.

Baada ya kupatiwa nyaraka za shauri hilo, wajibu maombi  wa kwanza (AG), kupitia kiapo na maelezo ya Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo na wajibu maombi wa pili mpaka wa tisa (mwenyekiti na wajumbe wa tume hiyo) nao katika  maelezo yao ya pamoja walipinga maombi hayo.

Wajibu maombi hao walipinga madai ya waombaji wakisema kuwa, Rais alitenda ndani ya mipaka ya sheria, yaani Sheria ya Tume za Uchunguzi (Sura ya 32 Toleo la Marejeo la 2023).

Pia, walijibu kuwa, madai ya waombaji dhidi ya makamishna ni dhana tu zisizo na ushahidi. Hivyo waliiomba Mahakama iyakatae maombi hayo.

Mjibu maombi wa kumi, Chama cha Sheria Tanganyika (TLS) kwa upande wake kupitia kiapo na maelezo ya  Katibu Mkuu Mtendaji wake, Mariam Othman kwa kiasi kikubwa alikubaliana na maombi ya waombaji.

 Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo Februari 26, 2026, mawakili wa waombaji, Hekima Mwasipu na Jebra Kambolewalifafanua kwa kina sababu za madai yao katika hati ya maombi na kiapo cha waombaji huku pia wakifanya rejea ya mashauri mbalimbali yaliyokwishakuamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Wajibu maombi wote AG na makamishna wa tume hiyo waliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method (PSA) akisaidiwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Daniel Nyakiha na Narindwa Sekimanga na Wakili wa Serikali, Erigh Rumisha huku yule wa TLS  akiwakilishwa na Ferdinand Makore na  Kulwa Shilemba.

Hoja za mawakili wa waombaji

Wakili Mwasipu akizungumzia uhalali wa tume hiyo, mbele ya Mahakama alidai kwamba, iliitwa kwa jina la “Tume Huru ya Kufanya Uchunguzi,” wakati sheria haitambui jina au cheo cha aina hiyo.

Alisema sheria inampa tu mamlaka Rais ya kuunda Tume ya Uchunguzi. Hivyo, alidai jina lilikuwa na kasoro kubwa iliyofanya tume hiyo kuwa batili.

Wakili Mwasipu alidai kuwa, kifungu cha 3(2) cha Sheria ya Tume za Uchunguzi kinaitaka mamlaka ya uteuzi wa tume kubainisha mada mahsusi ya uchunguzi na kwamba, katika shauri hilo mamlaka ya uteuzi ilitoa mada ambayo si mahsusi, hivyo kukiuka matakwa ya kifungu cha 3(2) cha sheria hiyo.

Pia, wakili Mwasipu alidai kuwa, tume hiyo  iliagizwa kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani, jambo ambalo kwa mujibu wa waombaji  halielezi kikamilifu wala kuakisi yaliyotokea.

Kwa maoni yake, maudhui ya uchunguzi yangefaa zaidi kama ingetamka kuhusu vifo, uharibifu wa mali za umma na binafsi, na kutoweka kwa watu kwa kulazimishwa.

Katika hoja nyingine kuhusiana na uhalali wa tume hiyo, Wakili Mwasipu alidai kuwa, wajumbe wa tume hiyo hawakuapishwa, hiyo ni kinyume na kifungu cha 7 cha sheria hiyo.

Vilevile alidai kuwa, mazingira yaliyosababisha kuundwa kwa tume hiyo hayakutangazwa katika Gazeti la Serikali, jambo ambalo ni kinyume pia na kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Tume za Uchunguzi.

Wakili Mwasipu pia alidai kuwa, uteuzi wa makamishna haukuwa wa busara wala wa mantiki.

Akifafanua, alisema uamuzi husemwa kuwa haukuwa wa busara pale mtu yeyote mwenye akili timamu asingefanya uamuzi huo au pale mamlaka inaposhindwa kuzingatia baadhi ya mambo muhimu.

Ili kuipa nguvu hoja yake hiyo, wakili Mwasipu aliielekeza Mahakama katika kesi mbalimbali ikiwamo ya Legal and Human Rights Centre na wengine wawili dhidi ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo na wengine watatu na shauri la madai namba 25 la 2018 la Mahakama Kuu Mtwara.

Akifafanua zaidi, wakili Mwasipu alidai uteuzi huo haukuwa wa busara kwa sababu wote walioteuliwa ni wastaafu na wenye umri zaidi ya miaka 60.

Badala yake, alidai kuwa mamlaka ya uteuzi ilipaswa kuzingatia na kujumuisha kizazi cha vijana na taasisi nyingine kama Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Katika hoja nyingine, wakili Mwasipu alidai kuwa tume inaonekana kuwa na upendeleo.

Wakili Mwasipu  alidai kuwa, mjibu maombi wa tisa (Tax)  ni waziri wa zamani wa ulinzi, wakati mjibu maombi wa saba (Mwema) ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu  (IGP).

Hivyo, alidai kuwa, mtu mwenye taarifa sahihi angeweza kudhani kuwa kuna upendeleo katika uteuzi wa wajumbe hawa.

Wakili Mwasipu alidai kwamba, wajumbe wote ni watumishi wa umma wastaafu na kwa sababu hiyo hawawezi kufanya uchunguzi dhidi ya mamlaka iliyowateua.

Pia, alidai kuwa katika machafuko hayo baadhi ya majengo ya Mahakama na vituo vya polisi vilichomwa moto, hivyo majaji wastaafu na maofisa wa polisi wastaafu (ambao ni wajumbe wa tume hiyo, hawakustahili kuwa wajumbe wa tume hiyo.

Kwa upande wake, wakili akizungumzia hoja ya matumizi mabaya ya mamlaka ya utashi katika uteuzi wa tume hiyo na nia mbaya.

Kwanza alidai kuwa, waombaji hawadai kwamba Rais hana mamlaka au hiari ya kufanya uteuzi, bali sheria inamtaka Rais kuteua watu wa makundi fulani, bali hoja yao ni matumizi yasiyofaa ya utashi wake.

Alifafanua kwamba, Rais aliteua watumishi wa umma pekee bila kujumuisha makundi mengine ili kusawazisha mizani ya haki.

Wakili Kambole alidai kuwa, Rais angeweza pia kuteua wajumbe wengine ambao hawana mgongano wa masilahi.

Kwa upande wake wakili wa TLS (mjibu maombi wa 10) aliunga mkono na kusisitiza hoja za mawakili wa waombaji.

‎Wakili Makore alidai kuwa, tume hiyo ni batili kwa kuwa haikutangazwa kwenye Gazeti la Serikali na wala wajumbe wa tume hiyo hawakula viapo kabla ya kuanza kazi yao kinyume na matakwa ya sheria.

Alidai kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi ili wajumbe wa tume wawe halali wanapaswa watangazwe katika Gazeti la Serikali.

‎Alifafanua kuwa, Amri C. 27 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 inataka machapisho na matangazo yote ya Serikali kuchapishwa na kutangazwa siku ya Ijumaa ya wiki husika.

‎Hata hivyo, alidai kuwa nakala ya gazeti lililowasilishwa na wajibu maombi kama kielelezo kuwa tume hiyo ilitangazwa si halali kwa kuwa limechapishwa Alhamisi, Novemba 20, 2025 hivyo kunaifanya tume hiyo kutokuwa halali.

‎Pia, wakili Makore alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha sheria hiyo ili wajumbe wa tume wawe halali wanapaswa kula viapo kwanza kabla ya kuanza majukumu yao.

‎Hata hivyo, alidai kuwa wajibu maombi katika majibu yao na viapo vyao kinzani hakuna mahali wanapoeleza kama walikula viapo wala kuambatanisha na fomu ya viapo.