SAFARI ya kinda wa Kitanzania, Gwakisa Mwakipesile imeanza kuonja ladha ya ushindani wa soka katika Ligi Kuu ya Vijana England baada ya kucheza mechi yake ya kwanza kwa walio na umri chini ya miaka 18.
Mwakipesile anayekipiga katika timu ya vijana ya Manchester Rose FC alipata nafasi ya kucheza Alhamisi wakati timu hiyo ilipokutana na Burnley FC katika mechi iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mwakipasile pamoja na Mtanzania mwenzie Calvin Emmanuel aliyekuwepo kikosini hapo tangu Januari mwaka huu, wote walianza kwenye kikosi hicho ingawa hawakufunga wala kutoa asisti.
“Tunafuraha kubwa kuwajulisha mchezaji wetu kinda, Gwakisa Mwakipesile, ametua salama jijini Manchester, England kwa ajili ya kuendelezwa kisoka katika timu ya vijana ya Manchester Rose FC,” ilisema taarifa hiyo
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa AYE sports kampuni iliyojikita kuendeleza vipaji vya vijana, kinda huyo alianza vizuri katika mchezo huo akijaribu kuendana na kasi ya soka la vijana nchini humo.
“Ni mwanzo mzuri kwake kucheza mechi yake ya kwanza. Alijitahidi kuonyesha uwezo wake na tunaamini ataendelea kuimarika kadri anavyoendelea kuzoea mazingira mapya,”
AYE inajivunia mafanikio ya kutoa vipaji hivyo kwani Mwakipasile anakuwa kijana wa pili kupata nafasi ya kwenda kuendelezwa England akifuata nyayo za Calvin Emmanuel.