*******
Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi katika Manispaa ya Lindi mkoani Lindi.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi Dkt. Stanford Mwakatage ambapo amesema kuwa kwa upande wa miundombinu ya barabara, kilomita 5.3 zitajengwa kwa kiwango cha lami ambapo licha ya kupendezesha mji, wananchi pia wataweza kupata huduma za usafiri kwa urahisi.
Kuhusu ujenzi wa stendi ya kisasa pamoja na soko la kisasa, kiongozi huyo amesema kuwa miradi hiyo itabadilisha kabisa mandhari ya manispaa ya Lindi na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja.
“Soko la kisasa linalojengwa litatumiwa na wafanyabiashara takribani 400 huku stendi mpya ikitarajiwa kupokea magari 80 kwa wakati mmoja na hii itakuza uchumi wetu na kuongeza mapato kwa manispaa yetu”, amesema Dkt. Mwakatege.
Naye, Meneja wa TARURA Manispaa ya Lindi Mhandisi Dawson Paschal amesema kuwa mradi wa TACTIC licha ya kuboresha barabara unalenga kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi hasa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa stendi katika eneo la Mitwero na kukamilika kwa soko jipya katika manispaa hiyo.
“Tunaipongeza Serikali kwa ujio wa mradi huu maana licha ya kuongeza mtandao wa barabara za lami mradi huu pia utapendezesha mji wetu wa Lindi na kuongeza kipato kwa mwananchi mmoja mmoja”, amesema Mhandisi Dawson.
Bi. Olivia Mwaipopo mkazi wa Manispaa ya Lindi amesema kuwa ujenzi wa stendi mpya ya Mitwero, ajira zimepatikana kwa akina mama na kwamba hata baada ya kukamilika, akina mama wataendelea kufanya biashara za kuuza chakula na bidhaa mbalimbali katika stendi hiyo mpya.
Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaotekelezwa kupitia mkopo nafuu toka Benki ya Dunia unaendelea kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuboresha miundombinu na kukuza uchumi wa wananchi.



