Global Publishers
March 16, 2026
0 Comments
Dar es Salaam, Machi 16, 2026 – Kampuni ya Coca-Cola Kwanza Ltd (CCK) imekabidhi Tuk-Tuk sita kwa wasambazaji bora wa bidhaa zake nchini kama sehemu ya programu ya motisha ya Returnable Glass Bottle (RGB) iliyofanyika katika robo ya nne ya mwaka uliopita.
Motisha hiyo ilikuwa wazi kwa wasambazaji wote waliokidhi vigezo vya kusambaza bidhaa za kampuni hiyo, ikiwa na lengo la kuhamasisha ukuaji wa biashara na kuhakikisha vinywaji baridi vinapatikana kwa urahisi kwa wateja katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Katika mpango huo, Tuk-Tuk nne zilitolewa kwa wasambazaji waliopata mauzo makubwa zaidi ya bidhaa za RGB katika robo ya nne ya mwaka, huku Tuk-Tuk mbili nyingine zikitolewa kwa wasambazaji waliorekodi mauzo makubwa zaidi ya RGB kwa mwaka mzima wa 2025.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Meneja Mkuu wa CCK, David Chait, alisema ushirikiano wa kampuni hiyo na wateja wake unalenga kuhakikisha kunakuwepo ukuaji wa pamoja wa biashara pamoja na kutoa thamani zaidi kwa walaji na washirika wa biashara.
Alisema kwa upande wa kampuni hiyo, kushirikiana na wateja kwa ajili ya ukuaji kunamaanisha kuelewa kwa kina mahitaji ya wateja na walaji, huku wakihakikisha wanatoa huduma bora zaidi ya kuuza vinywaji pekee.
Chait alieleza kuwa mpango wa Tuk-Tuk umetoa nafasi kwa wasambazaji wanaofanya vizuri kuimarisha biashara zao kwa kupata chombo cha ziada cha usambazaji, jambo linalosaidia kuhakikisha bidhaa zinapatikana kwa wakati, mahali sahihi na kwa bei inayofaa.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea kujenga ushirikiano imara na washirika wake wa biashara kuanzia maduka makubwa, wafanyabiashara wa kawaida, wauzaji wa jumla hadi maeneo ya burudani, kwa kuhakikisha utekelezaji bora wa huduma na utegemezi wa hali ya juu.