SERIKALI MKOA WA KAGERA KUENDELEA KUIUNGA MKONO TAAWANU KUWASAIDIA MAYATIMA

Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahaya Ramadhani Kido, imesema itaendelea kuiunga mkono Taasisi ya Taawanu katika juhudi zake za kuwajali watoto yatima ili kundi hilo lisijione kutengwa katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu huyo wa Mkoa mnamo Machi 15, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Zakat na Futari kwa watoto wanaolelewa katika vituo vya UYACHO na Nussuru Yatima. Hafla hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Kiislamu ya Taawanu Islamic Foundation na kufanyika katika ukumbi wa New HK Mexico uliopo Kashai.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Kido amepongeza juhudi za Taasisi ya Taawanu kwa kuwakumbuka watoto hao pamoja na watu wenye mahitaji maalum katika Mwezi mtukufu wa Ramadhani. Amesema kitendo hicho kina baraka nyingi na kinaimarisha mshikamano, upendo na faraja kwa watoto hao na kuwafanya wajione kuwa sehemu ya jamii.

 “Pamoja na kuwafuturisha watoto hawa, mmetoa pia Zakat na mitaji kwa watu wenye ulemavu. Nawapongeza sana kwa jambo hili jema na la mfano wa kuigwa. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Taasisi ya Taawanu, ili kuendelea kuyasaidia makundi yenye uhitaji katika jamii. Milango yetu iko wazi kwa ushirikiano huo,” amesema Kanali Kido.

Tukio hilo ni muendelezo wa shughuli mbalimbali za kijamii zinazofanywa na Taasisi ya Taawanu katika mikoa na nchi tofauti ndani na nje ya Bara la Afrika, zikiwa na lengo la kusaidia jamii kupitia matendo ya kheri.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na serikali pamoja na watu mashuhuri kutoka maeneo tofauti.