MABOSI wa Singida Black Stars, wameanza kumfuatilia kiungo mshambuliaji wa Gor Mahia FC ya Kenya, Mghana, Enock Morrison, ambaye hadi sasa hakuna mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya huko alipo, baada ya huu wa sasa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti, Enock ni miongoni mwa wachezaji wanaofuatiliwa kwa ukaribu na Singida, ambapo tayari mazungumzo ya mkataba huo wa awali yalianza kufanyika tangu kwenye dirisha dogo la Januari 2026.
Mtoa taarifa huyo, aliliambia Mwanaspoti, mmoja wa kiongozi aliyefanikisha usajili wa Elvis Rupia kujiunga na timu hiyo ndiye anayeshughulikia suala hilo, kutokana na ushirikiano mzuri aliokuwa nao na mchezaji na uongozi pia wa Gor Mahia.
“Ni mapema sana kuzungumzia hilo kwa sababu miezi mitatu iliyobakia lolote linaweza kutokea, sisi tunamsajili mchezaji mzuri kutokana na ripoti na mapendekezo ya benchi letu la ufundi, hivyo acha tuone mwisho wake,” kilisema chanzo hicho.
Mbali na hilo, vyanzo mbalimbali kutoka Ghana vinaeleza mchezaji huyo pia anafuatiliwa kwa ukaribu na vigogo wa soka hapa nchini Klabu ya Simba, ambayo imeonyesha uhitaji wa kumsajili, ingawa hakuna makubaliano rasmi yaliyowasilishwa mezani.
Nyota huyo aliyezaliwa Januari 18, 2000, akiwa na uwezo wa kucheza kiungo wa kati kwa ufasaha mkubwa, huku akitokea pia upande wa kulia na kushoto, amezichezea timu mbalimbali, zikiwamo King Faisal FC na Asante Kotoko zote za kwao Ghana.