Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliyohukumiwa watu wawili, baada ya kubaini kuwa ushahidi uliotumika kuwahukumu haukuthibitisha hatia yao bila kuacha shaka.
Walioachiwa huru ni Emmanuel Sayi na Yohani Emmanuel, ambao awali, wao na watu wengine watano, walikutwa na hatia ya kumuua Ester Kondela na kujaribu kumuua Leticia Daud.
Hukumu iliyowaachia huru warufani hao imetolewa Machi 13, 2026, na majaji watatu wa mahakama hiyo ambao ni Shaban Lila, Issa Maige na Latifa Mansoor, waliokuwa wakisikiliza rufaa ya jinai namba 256/2023.
Jaji Maige amesema baada ya kupitia mwenendo na sababu za rufaa, mahakama imejiridhisha kuwa utambulisho wa shahidi wa pili dhidi ya mrufani wa pili haukuwa wa kutegemewa, kwani ushahidi haukuweka wazi mwanga uliotumika kumtambua mrufani huyo.
Amesema mahakama pia ilitilia shaka ushahidi wa utambulisho uliotolewa na shahidi wa pili, ikisema kulikuwa na mashaka makubwa kuhusu uaminifu wa ushahidi wake.
Majaji walibaini kuwa kulikuwa na mkanganyiko kuhusu lini shahidi huyo alipata fahamu na lini alitoa taarifa yake kwa polisi, jambo lililoibua shaka juu ya usahihi wa utambulisho alioufanya.
Jaji Maige amesema mahakama pia ilieleza kuwa kulikuwa na mapungufu makubwa katika utambulisho wa simu, ikiwemo kutokuwepo kwa maelezo muhimu kama rangi ya simu au alama zilizotajwa baadaye mahakamani.
Majaji walieleza kuwa kukosekana kwa maelezo hayo katika nyaraka za awali kunaleta shaka kama simu iliyotolewa mahakamani ndiyo ile iliyodaiwa kuibiwa wakati wa tukio, ambapo iliamuliwa kuondoa simu hiyo kama kielelezo cha kesi hiyo.
Dosari nyingine ni kwamba mahakama ilibaini kuwa maelezo ya onyo ya warufani yalikuwa na tofauti na kutokubaliana kuhusu baadhi ya mambo muhimu ya tukio, ikiwemo idadi ya silaha zilizotumika na namna tukio lilivyotekelezwa.
Kutokana na tofauti hizo, majaji walieleza kuwa haikuwa salama kuyatumia maelezo hayo peke yake kama msingi wa kuwahukumu warufani bila ushahidi mwingine unaounga mkono.
Mahakama pia ilitathmini hoja ya upande wa mashtaka kuhusu kuwepo kwa mgogoro wa ardhi kati ya mmoja wa warufani na marehemu kama chanzo cha tukio.
Hata hivyo, ilibainika kuwa ushahidi kuhusu mgogoro huo haukuungwa mkono na vielelezo vya kutosha, kwani shahidi aliyedai kuripoti vitisho kwa polisi hakuwasilisha uthibitisho wowote wa taarifa hiyo.
Kutokana na mapungufu hayo ya ushahidi, mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha hatia ya warufani bila kuacha shaka, kama inavyotakiwa kisheria katika kesi za jinai.
Kwa msingi huo, mahakama ilibatilisha hukumu na adhabu zilizotolewa na Mahakama Kuu, na kuamuru warufani waachiliwe huru mara moja, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine za kisheria.
Awali, warufani hao walikuwa wakipinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Novemba 28, 2022. Katika kesi ya msingi, kosa la kwanza lilikuwa mauaji yaliyodaiwa kutokea Januari 2, 2016, katika mtaa wa Gitoya, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu, na kosa la pili likiwa ni kujaribu kumuua katika eneo hilohilo na tarehe hiyo.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 10 kutoka upande wa mashtaka na mashahidi wawili wa upande wa utetezi, Mahakama Kuu iliwakuta warufani na hatia na kuwahukumu adhabu ya kifo kwa kosa la mauaji pamoja na adhabu kwa kosa la jaribio la mauaji.
Hata hivyo, washtakiwa hao hawakuridhika na uamuzi huo na kuamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani, wakipinga ushahidi uliotumika kuwahukumu.
Katika hukumu yake, Mahakama ya Rufani ilieleza kuwa kesi ya awali ilitegemea zaidi ushahidi wa shahidi mmoja aliyenusurika katika tukio hilo, Leticia (shahidi wa pili), pamoja na ushahidi wa simu ya mkononi iliyodaiwa kuibiwa wakati wa tukio na baadaye kupatikana kwa mmoja wa warufani.
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, tukio hilo lilidaiwa kutokea usiku na watu hao waliokuwa na mapanga waliingia katika nyumba ambayo marehemu Ester alikuwa amelala pamoja na Leticia na kuwashambulia.
Shahidi wa pili alidai kuwa, kutokana na mwanga, alimtambua mmoja wa washambuliaji kuwa ni Yohani, ambaye ni binamu yake. Alidai washambuliaji hao walimshambulia marehemu kwa mapanga na kisha kumshambulia yeye pamoja na kumfanyia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kabla ya kupoteza fahamu kutokana na majeraha makubwa.
Uchunguzi wa kitabibu uliofanywa na daktari ulithibitisha kuwa marehemu alipata majeraha mengi ya kukatwa sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani na shingoni, ambayo yalisababisha kupoteza damu nyingi na hatimaye kufariki dunia.
Kwa upande wa Leticia, daktari alibaini kuwa alikuwa na majeraha makubwa ya kukatwa sehemu mbalimbali mwilini, pamoja na majeraha kichwani na mikononi.
Polisi walieleza kuwa, baada ya uchunguzi, walimkamata Yohani Emmanuel kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo kutokana na madai ya mgogoro wa ardhi kati yake na marehemu. Baadaye walimkamata Emmanuel na kudai kuwa alipatikana na simu ya mkononi iliyodaiwa kuibiwa kutoka kwa shahidi wa pili wakati wa tukio hilo.
Simu hiyo, aina ya Itel, ilitolewa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi, na upande wa mashtaka ulidai kuwa kupatikana kwa simu hiyo kwa mrufani wa kwanza kulionesha alihusika katika uhalifu huo.
Katika rufaa yao, mawakili wa warufani walipinga ushahidi huo, wakidai kuwa utambulisho wa simu hiyo haukuwa sahihi na kwamba mlolongo wa ulinzi wa kielelezo hicho haukufuatwa ipasavyo. Walidai kuwa kulikuwa na tofauti kubwa kati ya maelezo ya simu yaliyorekodiwa katika cheti cha kukamata na yale yaliyotolewa mahakamani na mashahidi.
