▪︎ Aagiza mradi ukamilike kwa wakati na ubora, asisitiza malipo kwa wafanyakazi wa mradi yafanyike kwa wakati
▪︎Awapongeza watumishi wa afya kwa weledi
Aidha, Waziri Mkuu amewapongeza watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahudumia wananchi na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kujituma.
Kadhalika, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye watumishi bora katika sekta ya afya katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), huku akisisitiza kuwa watumishi watakaobainika kufanya uzembe kazini watachukuliwa hatua stahiki.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, Dkt. Deogratias Banuba, amesema ujenzi wa jengo la huduma (Wing B) unagharimu takribani shilingi bilioni 13.28 na hadi sasa umefikia asilimia 59 ya utekelezaji.Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Februari 14, 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 13, 2026. Kukamilika kwa jengo hilo kutaiwezesha hospitali hiyo kuwa na wodi za kujifungulia, vyumba vya upasuaji pamoja na wodi ya kulaza watoto, ambazo kwa sasa hazipo.
Kwa mujibu wa Dkt. Banuba, huduma za kibingwa zinazotolewa katika hospitali hiyo ni pamoja na afya ya uzazi na mtoto, upasuaji, mifupa na ajali, masikio pua na koo, ganzi (Anesthesia), afya ya akili, macho, radiolojia pamoja na huduma ya uchujaji wa damu (Dialysis).Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Katavi, Mhe. Tasker Mbogo, aliwasilisha ombi kwa Waziri Mkuu akiomba Serikali ijenge eneo la kusubiria wagonjwa (waiting bay), chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na uzio wa hospitali hiyo.
Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Reuben Kwagila, amesema Serikali imepanga kupeleka takribani shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kuongezea majengo ya wodi, ujenzi wa chumba cha kuhifadhia maiti, ununuzi wa vifaa tiba pamoja na ujenzi wa uzio wa hospitali hiyo.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi na maeneo ya jirani, hususan huduma za mama na mtoto pamoja na huduma za kibingwa.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuhakikisha mradi huo unasimamiwa ipasavyo ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.