Dar es Salaam. Mashahidi 43, akiwemo Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Faustine Mafwele, wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi ya kughushi vibali vya kumiliki silaha inayowakabili watu tisa, wakiwemo maofisa sita wa Jeshi la Polisi.
Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Jumatatu, Machi 16, 2026, wakati akiwasomea hoja za awali (PH) washtakiwa hao.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mkaguzi wa Polisi mwenye namba PF.19931 Fredrick Malekela (45), mkazi wa Kilwa Road, E.4627 Sajenti Kalemwa Kaunga (54), mkazi wa Chanika, E.7855 Sajenti Edger Mlogo (54), mkazi wa Kibamba, F.1126 Sajenti Robert Titus (47), mkazi wa Kisarawe, F.5092 Sajenti John Kaposwe (46), mkazi wa Kurasini na WP 10050 Julieth Moshi (30), mkazi wa Kisarawe.
Wengine ambao si maofisa wa jeshi hilo ni Damson Mnyilenga (59), mkulima na mkazi wa Chanika, Simon Aloyce (60), mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza; pamoja na Venrand Liberio (29), mfanyabiashara na mkazi wa Tataba.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 16, yakiwemo ya kughushi vibali vya kumiliki silaha.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mwandamizi, Geofrey Mhini, na inatarajia kuanza kusikilizwa Aprili, 2026.
