KUELEKEA KUMBUKIZI- FAMILIA YA HAYATI JPM YAWASHIKA MKONO WAHITAJI

…………

CHATO

KUELEKEA kumbukizi ya miaka mitano ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, familia ndugu jamaa na marafiki wamefika hospitali ya wilaya ya Chato mkoani Geita kutoa matendo ya huruma pamoja na kuchangia damu kwaajili ya wahitaji.

Kabla ya kufika hospitalini hapo, familia na wadau wengine wakiongozwa na mtoto wa Hayati Dkt. Magufuli,(Jesca Magufuli) wamefanya matembezi ya hiari kutoka stendi ya zamani ya mabasi Muungano kuelekea hospitali ya wilaya hiyo.

Hatua hiyo imelenga kumuenzi Hayati Dkt. Magufuli kwa vitendo kutokana na falsafa yake ya kuwajali wananchi wasiojiweza na wanyonge.

Akizungumza wakati wa kukabidhi baadhi ya mahitaji kwa wagonjwa, Jesca amesema msaada huo ni mwendelezo wa matendo ya huruma yanayofanywa kila mara na familia ikiwemo wagonjwa, wafungwa na watu wasiojiweza.

Akishukuru kwa msaada huo, Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Chato, Dkt. Madili Sakumi, amesema hospitali hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa damu salama kutokana na jamii kutokuwa na mwamko wa kujitolea.

Hatua hiyo imekuwa ikisababisha maisha ya wagonjwa kuwa hatarini wakiwemo wajawazito, wenye ugonjwa wa seli mundu,Malaria pamoja na wanaopata ajali mbalimbali.

Mbali na hilo, Dkt. Sakumi amewasilisha maombi mbalimbali kwa familia na serikali kuu kusaidia ujenzi wa nyumba za watumishi kutokana na zilizopo kuwa chache na ambazo zilikuwa zikitumiwa na watumishi kingali bado kituo cha afya.

Vile vile suala ya uhaba wa uzio limetajwa kuwa changamoto inayosababisha baadhi ya wagonjwa kutoroko wodini na baadhi yao kuondoka pasipo kukamilisha malipo ya matibabu yao kinyume cha Sheria.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Tanzania bara, Mussa Mwakitinya, amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuzifanyia kazi changamoto zote za wananchi ikiwemo uhaba wa makazi ya wauguzi wa afya.

Ameahidi suala la uhaba wa nyumba za watumishi kwenye hospitali ya wilaya hiyo kuwa atalifikisha katika mamlaka zinazohusika ili liweze kutatuliwa.

Kadhalika Mwakitinya amewasisitiza wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali ili iweze kutekeleza miradi yote iliyoachwa na Hayati Dkt. Magufuli pamoja na mingine mipya kwa maslahi mapana ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, msafara huo mbali na msaada kwa wagonjwa, pia watu mbalimbali wamechangia damu ili kusaidia harakati za kunusuru afya za wagonjwa wenye uhitaji huo.