Wanawake na wasichana nchini wamehimizwa kutumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kwa njia sahihi ili kujijengea uwezo wa kiuchumi, kielimu na kijamii hatua itakayochangia kufikia malengo ya maendeleo ya taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2050.
Wito huo umetolewa na Kaim Mkurugenzi mtendaji wa shirika la CAMFED Tanzania Bi. Ana Sawaki kwenye kikao kazi Cha siku moja kilichoandaliwa na CAMFED kwa kushindana na Plan international chenye lengo la kuwajengea uwezo wasichana na wanawake katika masuala ya uongozi, usawa wa kijinsia pamoja na matumizi sahihi ya teknolojia na akili bandia (AI).
Kikao hicho kimefanyika makao makuu ya CAMFED kimewaleta pamoja wasichana na wanawake kutoka maeneo mbalimbali kwa lengo la kuimarisha uelewa wao kuhusu matumizi salama na yenye tija ya mitandao ya kijamii na teknolojia za kisasa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi huyo amesema kuwa mitandao ya kijamii na teknolojia za kidijitali zimefungua fursa kubwa za kujifunza, kufanya biashara na kupata taarifa muhimu, lakini pia zinaweza kuwa chanzo cha kupotoshwa au kuharibika kwa maadili endapo zitatumika vibaya.
Amesisitiza kuwa wasichana wanapaswa kujifunza na kutumia teknolojia kwa kuchagua maarifa sahihi yanayozingatia maadili na mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania.
“Mitandao ina fursa kubwa ya kujifunza, lakini pia ina hatari ya kuharibika kama haitatumika vizuri. Hivyo ni muhimu kwa wasichana kujifunza mambo sahihi yanayoendana na maadili ya nchi yetu na malengo ya maendeleo ya taifa,” alisema.
Aidha, amewahimiza wasichana na wanawake kufanya kazi kwa bidii na kujihusisha na shughuli za maendeleo zenye staha ili kujijengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Kwa mujibu wake, mwanamke anapokuwa na uwezo wa kiuchumi hupata nafasi kubwa ya kushiriki katika kufanya maamuzi ndani ya familia na jamii kwa ujumla.
“Wanawake wanapokuwa na uwezo wa kiuchumi wanapata nguvu ya kufanya maamuzi katika jamii. Hivyo ni muhimu kuwekeza katika elimu, ujuzi na teknolojia ili kuongeza uwezo huo,” aliongeza.
Katika mafunzo hayo pia ilielezwa kuwa dhana ya uwezeshaji wa wanawake (Women Empowerment) haipaswi kutafsiriwa kama ushindani dhidi ya wanaume, bali ni mchakato wa kumwezesha mwanamke kujitambua, kujenga uwezo wake na kutumia vipaji alivyonavyo kuchangia maendeleo ya jamii.
Washiriki wa kikao hicho walipata mafunzo mbalimbali ikiwemo matumizi sahihi ya akili bandia (AI), usalama wa mtandaoni, pamoja na namna teknolojia inavyoweza kuwa nyenzo muhimu katika kujenga uongozi wa wanawake na kukuza usawa wa kijinsia.
Shirika la CAMFED ambalo limekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza elimu ya wasichana barani Afrika, linaamini kuwa teknolojia ya kidijitali ni nyenzo muhimu katika kuwafikia wasichana wengi zaidi na kuwapa fursa za elimu, ajira na uongozi.
Navina Mutabazi ni mwezeshaji wanawake kidijitali anasema matumizi sahihi ya teknolojia kwa wasichana wanaweza kupata maarifa mapya, kuanzisha biashara za kidijitali, kujifunza stadi za kisasa pamoja na kushiriki katika mijadala ya maendeleo inayohusu taifa.
Hatua hivyo inaendana na mwelekeo wa maendeleo ya taifa unaolenga kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia, ubunifu na matumizi makubwa ya teknolojia kuelekea Tanzania yenye uchumi wa kisasa ifikapo mwaka 2050.
Kupitia programu zake za uongozi na uwezeshaji wa wasichana, CAMFED inaendelea kuwajengea uwezo wasichana na wanawake ili wawe viongozi wa sasa na baadaye, huku wakitumia teknolojia kama nyenzo ya kuharakisha maendeleo yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.
Mafunzo hayo pia yamewapa washiriki nafasi ya kujifunza namna ya kutumia teknolojia kwa uwajibikaji, kuzingatia maadili ya jamii na kuhakikisha kuwa maarifa wanayopata mtandaoni yanachangia maendeleo ya taifa.

