Na Mwandishi Wetu
LICHA ya wanawake kumiliki au kuendesha zaidi ya nusu ya biashara ndogo na za kati nchini, ushiriki wao katika nafasi za juu za maamuzi ndani ya taasisi za fedha bado uko chini ya asilimia 30, jambo linaloibua mjadala kuhusu usawa wa kijinsia katika sekta hiyo.
Hoja hiyo inatarajiwa kujadiliwa na wadau wa sekta ya fedha katika mkutano wa tatu wa Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha Tanzania (TAWiFA) utakaofanyika Machi 23, 2026 mjini Arusha.
Akizungumza leo Machi 16, 2026 kuelekea mkutano huo, Rais wa TAWiFA, Fikira Ntomola, amesema bado kuna changamoto zinazoathiri wanawake kupata fursa sawa katika sekta ya fedha, hasa katika nafasi za uongozi na upatikanaji wa huduma za kifedha.
“Pamoja na ongezeko la matumizi ya huduma za kifedha nchini, wanawake wengi bado wanakumbana na vikwazo vya kupata mikopo au mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao, hivi karibuni tutaanza utafiti kuangalia changamoto zinazowakabili wanawake kwenye msawala ya fedha ili waweze kuona namna ya kuwasaidia,” amesema.
Kwa mujibu wa utafiti wa FinScope Tanzania wa mwaka 2023, kiwango cha ujumuishaji wa kifedha nchini kimeongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita.
Takwimu zinaonyesha asilimia 76 ya Watanzania wazima sasa wanatumia huduma za kifedha, ikilinganishwa na takribani asilimia 16 mwaka 2009.
Hata hivyo, wadau wa sekta hiyo wanasema bado kuna pengo kati ya wanaume na wanawake katika kunufaika na baadhi ya huduma za kifedha, hususan mikopo ya biashara na uwekezaji.
Takwimu za taasisi za maendeleo ya biashara ndogo na za kati zinaonyesha kuwa wanawake wanamiliki au kuendesha zaidi ya asilimia 50 ya biashara ndogo na za kati nchini, sekta inayochangia kwa kiasi kikubwa katika ajira na ukuaji wa uchumi.
Katika ukanda wa Afrika Mashariki, tafiti zinaonyesha kuwa biashara zinazoendeshwa na wanawake zinachangia takribani asilimia 40 ya shughuli za kiuchumi, hali inayodhihirisha mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Hata hivyo, pamoja na mchango huo, ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za maamuzi ndani ya taasisi nyingi za kifedha bado ni mdogo,” amesema.
Utafiti uliofanywa na McKinsey & Company unaonyesha kuwa taasisi zenye uwiano mzuri wa kijinsia katika uongozi zina uwezekano mkubwa zaidi wa kufanya vizuri kiutendaji na kifedha kuliko zile zenye uwiano mdogo wa kijinsia.
Kwa upande wake, Meneja wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Bima Tanzania (Tira), Hadija Maulidi, alisema mkutano huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya fedha.
“Kwa upande wa bima ambayo ni sehemu ya sekta ya fedha, ushiriki wa wanawake unaendelea kuongezeka. Katika mkutano huu pekee zaidi ya wanawake 40 kutoka mamlaka yetu wanatarajiwa kushiriki,” ameongeza.
Pia amesema kupitia mamlaka hiyo wataendelea kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika soko la bima ili waweze kuchangia zaidi katika ukuaji wa sekta ya fedha na pia kushika nafasi za juu za uongozi.
Mbali na mkutano huo, waandaaji pia wanatarajia kutoa mafunzo ya elimu ya fedha kwa wanawake wajasiriamali 200 kabla ya mkutano huo. Baada ya mkutano, washiriki wanatarajiwa kushiriki zoezi la upandaji miti 2,000 katika shule 10 za msingi zilizochaguliwa mkoani Arusha.
Mkutano huo utawakutanisha wadau kutoka sekta za benki, bima, masoko ya mitaji, mifuko ya pensheni pamoja na mamlaka za udhibiti wa sekta ya fedha ili kujadili namna ya kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi wa sekta hiyo.