Serikali yatakiwa kutenga fedha za ukarabati wa majengo kila mwaka

Dar es Salaam.  Serikali imetakiwa kuweka utaratibu thabiti na wa kitaalamu wa kufanya ukarabati wa majengo ya taasisi za elimu kila mwaka ili kulinda uwekezaji mkubwa unaofanywa katika miradi ya maendeleo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko wakati kamati hiyo ilipokagua maendeleo ya ujenzi wa majengo manne katika Chuo Kikuu cha Ardhi unaotekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Sekiboko amesema ni muhimu Serikali kuweka mfumo wa mara kwa mara wa ukarabati wa majengo ili kuepusha hali ya kusubiri hadi miundombinu iharibike ndipo hatua zichukuliwe.

“Kama tunawekeza fedha nyingi kwenye miradi, ukarabati wake ufanyike kama inavyostahili sio hadi kusubiri ubovu utokee. Majengo yawekewe utaratibu mzuri wa kitaalamu wa ukarabati ikiwezekana kila bajeti,” amesema Husna.

Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa miradi mikubwa ya elimu inayotekelezwa kupitia HEET inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo vikuu nchini, hivyo ni muhimu pia kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa ili iweze kudumu kwa muda mrefu.

Ameeleza  kuwa, mara nyingi majengo mengi ya umma huanza kuharibika kwa sababu hayapati matengenezo ya mara kwa mara, jambo ambalo husababisha Serikali kutumia fedha nyingi zaidi kuyakarabati baada ya uharibifu kuwa mkubwa.

Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakikagua mojawapo ya majengo yaliyojengwa kupitia mradi wa HEET katika Chuo Kikuu Ardhi.

“Ni muhimu sana kuwa na mpango wa matengenezo ya kawaida. Hii itasaidia kulinda fedha za umma na kuhakikisha majengo yanaendelea kutumika kwa ufanisi kwa muda mrefu,” amesisitiza.

Kuhusu hatua ya utekelezaji wa mradi huo amesema kamati imeridhishwa na kasi ya ujenzi ambayo imefikia asilimia 99 ambapo kukamilika kwake kunatarajiwa kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa chuoni hapo, kuboresha miundombinu ya kufundishia, kufanya tafiti na kujenga uwezo wa kitaaluma.

Katika chuo hicho mradi huo unahusisha ujenzi wa majengo mapya ya kufundishia pamoja na miundombinu ya kisasa inayotarajiwa kuongeza uwezo wa chuo kupokea wanafunzi wengi zaidi na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

“Umuhimu wa chuo hiki unaenda kuongezeka maradufu, kwa uwekezaji huu tunategemea kuongeza wigo wa udahili wa wanafunzi na kuleta tija kwenye jamii.

“Ni imani yetu kwamba chuo hiki sasa kitatusaidia kutatua changamoto zote za ardhi zinazoendelea kwenye nchi yetu, maeneo mengine unakuta kuna changamoto ya mipaka ya wilaya na wilaya au mkoa kwa mkoa wataalamu hawa wakatusaidie,” amesema.

Sekiboko amesema kamati itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo zinatumika ipasavyo na kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Amesisitiza  kuwa, uwekezaji katika elimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa, hivyo ni lazima miradi inayotekelezwa isimamiwe vizuri kuanzia ujenzi hadi matengenezo ya baadaye.

Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa ameahidi kuzingatia ushauri uliotolewa na kamati hiyo, huku ukieleza kuwa chuo kinaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi wa huo ili kuhakikisha unakamilika kwa ubora na kwa wakati uliopangwa.

Kwa chuo hicho mradi unahusisha ujenzi wa majengo manne ambayo ni maabara saba, jengo la studio lenye vyumba 15, karakana 10 na madarasa 26.

Profesa Liwo amesema ujenzi huo utakapokamilika majengo hayo yatakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 6,956 na watumishi 73.