Serikali kuendelea kupeleka  wanafunzi nje kusomea AI

Dar es Salaam. Katika wakati ambao dunia inaingia kwa kasi katika mapinduzi ya teknolojia ya akili unde, Serikali imebainisha kuwa itachukua hatua za makusudi kuhakikisha Tanzania haibaki nyuma katika ushindani wa maarifa na teknolojia.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda amesema Serikali imeanza kampeni ya kuandaa wataalamu wa teknolojia hizo kwa kuwapeleka wanafunzi kusoma katika vyuo vya nje ya nchi, sambamba na kuimarisha uwezo wa ndani wa kufundisha na kufanya tafiti.

Profesa Mkenda amesema hayo leo Machi 16,2026 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo ilipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (COICT) chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya kiuchumi (HEET).

Akizungumzia hatua hizo, Profesa Mkenda amesema tayari wahitimu 16 wamepelekwa Afrika Kusini kusoma masomo yanayohusiana na akili unde na sayansi ya data, huku wengine 34 wakitarajiwa kwenda nchini Ireland kwa ajili ya mafunzo hayo.

Amesema licha ya jitihada za kujenga uwezo wa ndani, bado ni muhimu wanafunzi wa Kitanzania kupata uzoefu wa kimataifa katika maeneo ya teknolojia yanayokua kwa kasi.

“Kwa sasa tunaendelea kujenga uwezo wa ndani lakini hilo halitufanyi tusipeleke wanafunzi nje kwa ajili ya kupata ujuzi na uzoefu zaidi katika teknolojia hizi,” amesema.

Profesa Mkenda amesema maendeleo ya teknolojia ya akili unde yana faida nyingi katika maendeleo ya jamii na uchumi, lakini pia yana changamoto ambazo ni muhimu jamii ikazifahamu mapema.

Amesema baadhi ya changamoto zinazoonekana kwa sasa ni pamoja na matumizi mabaya ya teknolojia hiyo katika kutengeneza picha au video zisizo halisi, ingawa amesisitiza kuwa changamoto hiyo si kubwa ikilinganishwa na athari nyingine zinazoweza kujitokeza.

Amesema changamoto kubwa zaidi ni uwezekano wa baadhi ya kazi kupotea kutokana na mashine na mifumo ya kidijitali kufanya kazi ambazo hapo awali zilifanywa na binadamu.

Amesema pamoja na kupungua kwa baadhi ya ajira, teknolojia hiyo pia itafungua fursa mpya za kazi ambazo zitahitaji wataalamu wenye ujuzi maalumu.

“Teknolojia inaweza kusababisha baadhi ya watu kupoteza kazi, lakini pia inaleta fursa mpya za ajira ambazo zinahitaji maandalizi makubwa ya rasilimali watu,” amesema.

Aidha, Profesa Mkenda amesisitiza  umuhimu wa wananchi kulinda taarifa zao binafsi, akieleza kuwa mifumo mingi ya akili unde hutegemea taarifa zinazopatikana kwenye mtandao.

“Kwa kiasi kikubwa akili unde hutumia taarifa zilizopo mtandaoni, hivyo ni muhimu watu kulinda taarifa zao binafsi,” amesema.

Hatua hizo za Serikali zinaenda sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya kujifunzia, ikiwamo ujenzi wa jengo jipya la ICT Complex katika ndaki hiyo ya Tehama litakaloongeza uwezo wa udahili na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Jengo hilo litakuwa na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 140, karakana mbili zenye uwezo wa wanafunzi 30 kila moja pamoja na maabara mbili zitakazoweza kuhudumia jumla ya wanafunzi 96.

Pia, litakuwa na studio, ukumbi mdogo wa mikutano pamoja na ofisi 20 zitakazotumiwa na wafanyakazi 43.

Rasi wa ndaki hiyo  Profesa Baraka Maiseli amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wapya 351 na kuboresha ubora wa wahitimu kutokana na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kujifunzia na kufundishia.

Aidha, miundombinu hiyo itatoa nafasi ya kuanzishwa kwa programu mpya 10 za masomo, ikiwamo programu ya ulinzi wa taarifa inayolenga kuandaa wataalamu wa usalama wa taarifa za kidijitali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge Husna Shekiboko amesema ujenzi wa jengo hilo ni miongoni mwa miradi michache waliyoikagua na kukuta ikiendelea vizuri bila changamoto zilizosababisha mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji.

Akitoa maoni yake, mbunge wa viti maalumu Asha Feruzi ameitaka  Serikali kupanua wigo wa ushirikiano na nchi zilizoendelea katika teknolojia ya akili unde ili wanafunzi wa Tanzania wapate fursa zaidi za mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Mratibu wa mradi wa HEET UDSM, Profesa Benadeta Killian amesema ndaki hiyo ina mpango wa kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Akili Unde kitakachosaidia kufanya tafiti na kutoa mafunzo ya juu katika teknolojia hiyo.

Amesema katika  kipindi hiki cha mageuzi makubwa ya teknolojia duniani, taasisi za elimu ya juu hazina budi kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko hayo ili kuandaa wataalamu watakaoweza kukidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye.