Wawili wafa ajali ya jahazi Nungwi, watatu hawajulikani walipo

Kigoma/Tanga.  Wakati mwili wa aliyekuwa mtumishi wa afya, Amos Sika (33), ukipatikana, watu wawili wamefariki dunia na watatu hawajulikani walipo baada ya jahazi kuzama eneo la Nungwi kwenye Bahari ya Hindi.

Sika alifariki dunia katika ajali ya boti ya Ziwa Tanganyika  iliyotokea Machi 13, 2026 ikiwa imebeba watu 19 wakiwamo watumishi wa afya, wahamasishaji wake huku 11 kati yao wakinusurika kifo.

Juzi, Machi 14, 2026 ilitokea ajali ya jahazi la kubeba mizigo lililokuwa likisafiri kutoka Bandari ya Pangani mkoani Tanga kwenda Bandari ya Mkokotoni kisiwani Unguja.

Jahazi hilo mbali na kubeba mizigo pia lilikuwa na watu 12 wakiwamo abiria tofauti na sheria inavyowataka.

Kaimu Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mhandisi Christopher Mlelwa leo Machi 16, 2026, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Mlelwa amesema jahazi hilo lililozama linajulikana kwa jina la MV Talawanda na lilikuwa likifanya safari zake za kusafirisha mizigo kati ya Pangani (Tanga) na Mkokotoni (Unguja).

“Kimsingi tunasisitiza vyombo vyote vinavyosafiri kwa njia ya maji vinatakiwa kusajiliwa na kuthibitishwa ubora na mamlaka husika ambayo ni Tasac,” amesema Mlelwa.

Pia, amesema chombo hicho kilikuwa kimesajiliwa kwa ajili ya kubeba mizigo pekee na si abiria.

Kaimu Afisa Mfawidhi wa Shirika la Utawala wa Meli Tanzania TASAC Mhandisi, Christopher Mlelwa akizungumza na waandishi wa habari katika Bandari ya Pangani mkoani Tanga jitihada zinazoendelea za kuwatafuta watu watatu wa ajali ya jahazi Nungwi ambao hawajulikani waliopo.

“Chombo ambacho kilipata ajali Machi 14 kilisajiliwa kwa ajili ya mizigo, kilitoka Bandari ya Pangani kwenda Mkokotoni, lakini kilipoteza mwelekeo kutokana na hali mbaya ya hewa,” amesema.

Amesema manahodha wa chombo hicho hawakuzingatia tahadhari za utabiri wa hali ya hewa ambao mamlaka zimekuwa zikisisitiza mara kwa mara kwa wasafiri wa majini.

Kwa mujibu wa taarifa za Bandari ya Pangani, jahazi hilo lilianza safari likiwa na wafanyakazi sita pekee.

Hata hivyo, baada ya ajali ilibainika kulikuwa na watu zaidi ndani ya chombo hicho kuliko waliokuwa wameanza safari.

“Baada ya ajali ilibainika kuwa chombo hicho kilikuwa na watu 12, wakiwamo mabaharia na abiria watano waliopandishwa njiani,” amesema Mlelwa.

Amesema abiria hao wanadaiwa kupandishwa eneo la Ushongo Pangani, bila kufuata utaratibu wa usafiri wa majini.

“Kimsingi chombo hicho kilikiuka utaratibu kwa kubeba abiria wakati kilisajiliwa kwa ajili ya kubeba mizigo,” amesisitiza.

Mlelwa amesema operesheni ya utafutaji na uokoaji ilifanywa na Kikosi cha KMKM cha Zanzibar kwa kushirikiana na manahodha wa boti kutoka Ushongo na maeneo mengine ya Pangani.

“Kwa taarifa tulizopata kutoka kituo cha utafutaji na uokoaji MRCC, watu saba waliokolewa katika ajali hiyo,” amesema.

Amesema hadi sasa watu watatu bado hawajaonekana huku miili miwili ikiwa tayari imepatikana eneo la Mkokotoni.

Mmoja wa wamiliki wa jahazi eneo la Pangani, Mngwali Usi amesema mara nyingi ajali za majini hutokana na tamaa ya kupakia mizigo kupita uwezo wa chombo.

“Wakati mwingine ukiwaambia manahodha wasipakie zaidi ya kiwango hawasikii kwa sababu ya tamaa ya fedha,” amesema.

Majajazi yakiwa yameegeshwa katika Bandari ya Pangani yakisubiria muda wa kipakia mizigo kwa ajili ya safari ya Mkokotoni Unguja

Amesema yeye hulazimika kwenda mwenyewe bandarini kusimamia upakiaji wa mizigo ili kuhakikisha hauzidi uwezo wa chombo.

Mmiliki huyo amesema siku ya tukio alizungumza na mmoja wa mabaharia aliyefariki dunia ambaye ni mtoto wa dada yake.

“Yule aliyekufa ni mtoto wa dada yangu, nilimwambia mara nyingi bahari si ya mchezo kwa vijana wadogo, lakini wakati mwingine wanakucheka wakisema mzee umepitwa na wakati,” amesema Usi.

Pia, amesema siku hiyo hali ya hewa haikuwa nzuri na aliwashauri baadhi ya manahodha kusubiri au kuelekea bandari nyingine salama.

“Nilimwambia aende hadi Bandari ya Kikubwi kwa sababu hali ya hewa haikuwa nzuri, lakini mwenzake aliyekuwa naye hakusikia na akaendelea na safari,” amesema Usi.

Amesema baadaye alijaribu kuwapigia simu kuwaonya zaidi kuhusu hali ya hewa lakini simu zao zilikuwa zimezimwa.

“Nilijaribu kuwapigia simu kuwaambia hali ya bahari si nzuri, lakini simu zao zilikuwa zimezimwa wakiamini watafika salama,” amesema.

Baharia wa Jahazi la Subira, Juma Mashali amesema wakati mwingine changamoto hutokana na shinikizo la wafanyabiashara wanaotaka mizigo yao ifike haraka.

“Wakati mwingine wafanyabiashara wanalazimisha mizigo yao isafirishwe hata kama hali ya hewa si nzuri,” amesema.

Amesema katika mazingira kama hayo manahodha hulazimika kufanya uamuzi mgumu ili kulinda usalama wa watu.

Mashali amesisitiza umuhimu wa mabaharia na manahodha kupewa mafunzo ya kutosha pamoja na kufuata utabiri wa hali ya hewa ili kuepusha ajali za majini.