JAI yapanga kulisha wagonjwa zaidi ya 1,800 Eid El-Fitr, yaomba msaada wa Sh. Milioni 22

Taasisi ya Jumuiya ya Tabia za Kiislam (JAI ) imepanga kuwalisha wagonjwa zaidi ya 1,800 katika hospitali mbalimbali wakati wa sikukuu ya Eid al‑Fitr, ikiwa ni sehemu ya kuwafariji na kuwafanya wajione kuwa ni sehemu ya jamii licha ya changamoto za kiafya wanazopitia.

Akizungumza katika hafla ya uchangiaji iliyoandaliwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo, Katibu wa JAI, Ramadhani Kombo, amesema jumuiya hiyo imejipanga kuhakikisha wagonjwa wanasherehekea sikukuu hiyo kwa furaha kama Watanzania wengine.

Amesema matarajio yao ni kuwafikia wagonjwa zaidi ya 1,800 kwa kuwapatia chakula maalum cha sikukuu, huku makadirio ya bajeti ya kufanikisha zoezi hilo yakifikia shilingi milioni 22.

“Tumekutana hapa kuhamasisha wadau na watu wenye mapenzi mema kujitokeza kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha zoezi hili. Lengo letu ni kusherehekea sikukuu pamoja na wagonjwa ili nao wajione ni sehemu ya Watanzania, kwani maradhi ni mitihani ya maisha,” amesema Kombo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JAI, Ridhiwani Mpanju amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2008 kabla ya kusajiliwa rasmi mwaka 2014, ikiwa na dhamira ya kuwahudumia wagonjwa na kuwapa faraja katika kipindi wanachopitia changamoto za kiafya.

Amesema kupitia makao makuu ya jumuiya hiyo yaliyopo Magomeni, wamekuwa wakitekeleza shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwapatia wagonjwa uji wa asubuhi na chakula cha kufuturu wakati wa mwezi wa Ramadhani, pamoja na kusaidia kulipia bili za wagonjwa waliokwama hospitalini.

Ameongeza kuwa katika kusherehekea Eid al‑Fitr mwaka huu, jumuiya hiyo imepanga kuandaa chakula maalum na kula pamoja na wagonjwa hao ili kuwapa faraja na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa na jamii.

Kutokana na mpango huo, viongozi wa jumuiya hiyo wamewaomba waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuchangia ili kufanikisha lengo la kuwafikia wagonjwa hao zaidi ya 1,800 siku ya sikukuu.