Hofu yatanda Hormuz ikifungwa, Marekani yaita washirika kuifungua

Tokyo. Wakati Iran ikiapa kuzuia meli za mafuta kupita katika Mlango Bahari wa Hormuz, Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa wito kwa nchi washirika kushiriki katika kulinda na kufungua tena njia hiyo ya bahari, hata hivyo mwitikio kutoka kwa baadhi ya washirika wakuu umekuwa mdogo.

Nchi kama Japan na Australia zimesema hazina mpango wa kutuma meli za kivita Mashariki ya Kati kusindikiza meli za mafuta kupitia njia hiyo muhimu ya usafiri wa nishati duniani.

Mlango huo wa bahari una kina kinachotosha kuruhusu meli kubwa zaidi duniani za kusafirisha mafuta kupita. Pia, hutumiwa na wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi Mashariki ya Kati pamoja na wanunuzi wao duniani.

Sehemu ya Mlango Bahari wa Hormuz ambao una kina kinachotosha kuruhusu meli kubwa zaidi duniani za kusafirisha mafuta kupita.

Wito huo wa Trump unakuja wakati vita kati ya Israel, anayeshirikiana na Marekani, dhidi ya Iran ikiingia wiki ya tatu na kusababisha misukosuko katika Mashariki ya Kati pamoja na kuyumbisha masoko ya nishati duniani.

Akizungumza jana Jumapili, Trump amesema mataifa yanayotegemea kwa kiasi kikubwa mafuta kutoka Ghuba ya Uajemi yana wajibu wa kulinda mlango huo wa bahari, ambako takribani asilimia 20 ya nishati ya dunia hupita.

Masoko ya Asia yalionesha tahadhari huku bei ya mafuta ghafi ya Brent ikipanda zaidi ya asilimia moja hadi kufikia zaidi ya Dola 104.50 za Marekani kwa pipa.

Masoko mengi ya hisa katika eneo hilo pia yalishuka kutokana na hofu ya athari za vita kwenye miundombinu ya mafuta ya Mashariki ya Kati na wito wa Trump kwa washirika kuongeza ushiriki wao.

“Ninadai nchi hizi zije kulinda eneo lao wenyewe kwa sababu ni eneo lao,” Trump amewaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege ya Rais Air Force One, akitokea Florida kuelekea Washington. “Hapo ndipo wanapopata nishati yao.”

Trump amesema utawala wake umefikia nchi saba, lakini hakuzitaja. Katika ujumbe wa mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki, ameonesha matumaini kuwa China, France, Japan, Korea Kusini, Uingereza na mataifa mengine yatahusika katika kulinda njia hiyo.

Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, ambaye anatajwa kuwa mshirika wa karibu wa Trump, amesema nchi yake haina mpango wa kutuma meli za kivita kulinda meli Mashariki ya Kati, ambako Japan hupata takribani asilimia 95 ya mafuta yake.

“Hatukufanya uamuzi wowote kuhusu kutuma meli za kusindikiza. Tunaendelea kuchunguza kile ambacho Japan inaweza kufanya ndani ya mfumo wa sheria uliopo,” amesema bungeni.

Kwa upande wake, Australia, mshirika muhimu wa usalama wa Marekani katika eneo la Indo-Pasifiki, pia ilisema haitatuma meli zake za kivita kusaidia kufungua njia hiyo.

Waziri katika serikali ya Waziri Mkuu, Anthony Albanese, Catherine King, amesema katika mahojiano na shirika la utangazaji la Australian Broadcasting Corporation kuwa Australia haijaombwa kufanya hivyo na haina mpango wa kuchangia operesheni hiyo.

Trump pia amesema anaweza kuahirisha ziara yake iliyopangwa mwishoni mwa mwezi huu kwenda Beijing kukutana na Rais wa China, Xi Jinping, ikiwa Beijing haitasaidia katika juhudi za kufungua njia hiyo ya bahari.

“Nadhani China pia inapaswa kusaidia kwa sababu inapata asilimia 90 ya mafuta yake kupitia mlango huo,” amesema Trump katika mahojiano na gazeti la Financial Times.

Wakati huohuo, mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) wanatarajiwa kujadili uwezekano wa kuimarisha operesheni ndogo ya kijeshi ya majini ya umoja huo katika Mashariki ya Kati, ingawa wanadiplomasia wanasema huenda wasifanye uamuzi wa kupanua jukumu lake hadi katika Mlango wa Hormuz.

Rais wa Marekani, Donald Trump.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, pia amejadiliana na Trump kuhusu umuhimu wa kufungua njia hiyo ya bahari, pamoja na mazungumzo aliyofanya na Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney.

Safari za ndege zatatizika

Wakati huohuo, vita vinavyoendelea dhidi ya Iran vimesababisha usumbufu mkubwa katika usafiri wa anga duniani, baada ya baadhi ya vituo muhimu vya ndege Mashariki ya Kati, kama Dubai, Doha na Abu Dhabi, vikifungwa au kuweka vikwazo vya safari za ndege.

Mashirika ya ndege yamelazimika kufuta maelfu ya safari, huku maelfu ya abiria wakikwama katika viwanja vya ndege.

Mamlaka nchini Vietnam pia zimeonya sekta ya anga kujiandaa na uwezekano wa kupunguza safari za ndege kuanzia Aprili, baada ya China na Thailand kusitisha usafirishaji wa mafuta ya ndege kutokana na vita hivyo.

Katika tukio jingine, mamlaka ya Dubai zimedhibiti moto uliosababishwa na shambulizi la droni lililolenga tanki la mafuta karibu na uwanja wa ndege, hatua iliyosababisha kusitishwa kwa muda kwa safari za ndege.

Nchini Saudi Arabia, vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa droni 34 zilidunguliwa ndani ya saa moja katika eneo la mashariki mwa nchi. Hakuna majeruhi yaliyoripotiwa.

Licha ya madai ya Marekani kuwa imeharibu uwezo wa kijeshi wa Iran, mashambulizi ya droni bado yanaendelea kutishia nchi za Ghuba.

Wakati huohuo, maofisa wa Marekani wamesema wanatarajia vita dhidi ya Iran kumalizika ndani ya wiki chache zijazo na bei za nishati kushuka.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amepinga madai ya Trump kuwa nchi yake inataka mazungumzo.

“Hatujawahi kuomba kusitishwa kwa mapigano, wala hatujaomba hata mazungumzo,” amesema katika kipindi cha Face the Nation cha kituo cha televisheni cha CBS. “Tuko tayari kujilinda kwa muda wowote utakaohitajika.”

Mlango wa Bahari wa Hormuz ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za usafirishaji duniani na pia ni moja ya maeneo nyeti zaidi ya kupitisha mafuta ghafi.

Ukanda huo wa bahari unapakana na Iran upande wa kaskazini na Oman pamoja na Falme za Kiarabu (UAE) upande wa kusini. Njia hiyo, yenye upana wa takribani kilomita 50 katika sehemu za kuingia na kutoka, na takribani kilomita 33 katika sehemu yake nyembamba zaidi, inaunganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Kiarabuni.

Mlango huo wa bahari una kina kinachotosha kuruhusu meli kubwa zaidi duniani za kusafirisha mafuta kupita. Pia, hutumiwa na wazalishaji wakubwa wa mafuta na gesi Mashariki ya Kati pamoja na wanunuzi wao duniani.

Mwaka 2025, takribani mapipa milioni 20 ya mafuta yalipita kupitia Mlango Bahari wa Hormuz kila siku, kwa mujibu wa makadirio ya Taasisi ya Marekani ya Usimamizi wa Taarifa za Nishati. Hiyo ni sawa na biashara ya nishati yenye thamani ya karibu Dola 600 bilioni kwa mwaka.

Mafuta hayo hayatoki Iran pekee, bali pia kutoka nchi nyingine za Ghuba, Iraq, Kuwait, Qatar, Saudi Arabia na UAE.

Kwa kawaida, takribani meli 3,000 hupita katika mlango huo wa bahari kila mwezi.

Hata hivyo, tangu kuanza kwa vita dhidi ya Iran, bei za nishati zimepanda kwa kasi na kubadilika-badilika. Bei ya mafuta ilikaribia kufikia Dola 120 kwa pipa jana Jumatatu kabla ya kushuka tena, ingawa bado iko juu zaidi kuliko viwango vilivyokuwepo kabla ya mzozo huo.

Kwa mujibu wa takwimu za London Stock Exchange Group, gharama ya kukodi meli kubwa ya kubeba mafuta (supertanker) kusafirisha mafuta kutoka Mashariki ya Kati kwenda China imeongezeka karibu mara mbili ikilinganishwa na wiki iliyopita, na kufikia rekodi mpya ya zaidi ya dola 400,000 kwa safari.

Kufungwa kwa kiasi kikubwa kwa njia hiyo muhimu ya usafirishaji pia kumeathiri nchi za Ghuba, kama Saudi Arabia, ambazo uchumi wake unategemea kwa kiwango kikubwa mauzo ya nishati nje ya nchi.