Dar es Salaam, Tanzania.
WANAAWAKE wafanyakazi wa Airtel Tanzania kupitia kundi lao la Airtel Divas wametembelea kituo cha kulea watoto wenye mtindio wa ubongo kinachoendeshwa na Dorcas Foundation kilichopo Madale jijini Dar es Salaam, na kutoa msaada kwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea msaada huo, Meneja wa Programu wa Dorcas Home Care, Lisa Mbukilo, amesema kituo hicho kinaendelea kuona maendeleo ya kutia moyo kwa baadhi ya watoto wanaopatiwa huduma za matibabu na uangalizi. “Kati ya zaidi ya watoto 70 wanaolelewa kupitia Dorcas Foundation, takribani watoto 20 walioanza kupata huduma katika kituo hiki wameanza kuonesha maendeleo mazuri ikiwemo uwezo wa kutembea kwa msaada pamoja na kufanya baadhi ya shughuli ndogo za kila siku, jambo linalotoa matumaini kwa wazazi na walezi kuwa wanaweza kurejea katika hali bora zaidi kiafya,” amesema.
Mbukilo ameongeza kuwa licha ya maendeleo hayo, kituo hicho bado kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa bima za afya, dawa pamoja na vifaa tiba vinavyohitajika ili kusaidia matibabu na uangalizi wa watoto zaidi ya 70 waliopo katika kituo hicho.
Kwa upande wake, kiongozi wa msafara wa Airtel Divas kutoka Airtel Tanzania, Jemima Masimba, amesema ujio wao katika kituo hicho unaonesha dhamira ya wanawake wa Airtel kurudisha kwa jamii kwa kusaidia makundi yenye uhitaji maalum. “Kama wanawake wa Airtel Tanzania tunaamini katika kusaidia jamii na kuunga mkono juhudi zinazotoa matumaini na kuleta mabadiliko chanya. Kupitia ziara hii tumetoa msaada pamoja na kushiriki katika kampeni ya Kibubu cha Dorcas inayohamasisha wadau mbalimbali kuchangia ili kuwezesha ununuzi wa eneo kwa ajili ya kituo cha kudumu cha kulea watoto wenye mtindio wa ubongo,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Dorcas Foundation, Rehema Semfukwe, amewashukuru wanawake wa Airtel Tanzania kwa kutembelea kituo hicho na kuunga mkono kampeni ya Kibubu cha Dorcas. “Tunawashukuru sana wanawake wa Airtel Tanzania kwa kutuunga mkono katika kampeni hii ambayo inalenga kutuwezesha kununua eneo kwa ajili ya kituo cha kudumu kitakachotusaidia kupanua huduma na kuendelea kuwahudumia watoto wenye mtindio wa ubongo,” amesema.
Mpango wa Airtel Divas unawakutanisha wanawake wafanyakazi wa Airtel Tanzania wanaoshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kusaidia jamii na makundi yenye uhitaji maalum.

.jpeg)
.jpeg)
