Mwenyekiti wa kijiji mbaroni kwa madai ya kumpa ujauzito mwanafunzi

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlangoni, Wilaya ya Siha mkoani humo, Ezekiel Mloli kwa madai ya kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne katika moja ya shule za sekondari wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Christopher Timbuka amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akidai mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa mahojiano.

“Ni kweli tukio hili limetokea katika Kijiji cha Mlangoni, Kata ya Gararagua na mtuhumiwa alikamatwa na kuhojiwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” amesema Timbuka.

Kamanda wa Polisi Mkoa, Simon Maigwa amethibitisha kukamatwa kwa mwenyekiti huyo akisema taratibu za kisheria zitakapokamilika kesi itafikishwa mahakamani.

“Baada ya taarifa kutolewa kwa uongozi wa shule, mwathirika alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Siha kwa uchunguzi wa kitabibu, ilibainika mwanafunzi huyo ana ujauzito wa wiki 17 na siku moja,” amesema Kamanda Maigwa.

 “Baada ya uchunguzi huo wa kitabibu, mwathirika alihojiwa na kueleza kuwa mhusika wa ujauzito ni mwenyekiti wa Kijiji cha Mlangoni.”

 Kamanda Maigwa amesema baada ya mahojiano jalada la shauri hilo linaandaliwa ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.