Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Kimira, Kata ya Romu, Wilaya ya Hai, Juma Kimaro (36), kwa tuhuma za kumuua mfanyabiashara Sakina Paulo Tarimo (68).
Inadaiwa mtuhumiwa huyo alikuwa akimtuhumu marehemu kujihusisha na imani za kishirikina, akidai kuwa alikuwa akiwaloga watoto wake.
Akithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo leo, Machi 16, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Simon Maigwa, amesema mtuhumiwa alikamatwa mkoani Dodoma alipokuwa amejificha, baada ya kufanya tukio hilo Machi 2 mwaka huu.
Kamanda Maigwa amesema mtuhumiwa anadaiwa kumvamia mfanyabiashara huyo nyumbani kwake dukani na kumjeruhi kwa kutumia kitu chenye ncha kali kinachodaiwa kuwa panga, na kusababisha kifo chake.
“Machi 2, 2026, usiku, katika Kijiji cha Kimira, Kata ya Romu, mfanyabiashara Sakina Paulo Tarimo (68) aliuawa kwa kukatwa sehemu mbalimbali za mwili na mtu asiyejulikana, baada ya kuvamiwa akiwa dukani kwake,” amesema Maigwa.
Amesema wakati tukio hilo likitokea, mjukuu wa marehemu alikuwa jikoni akipika maandazi na alisikia kelele za bibi yake akiomba msaada. Mjukuu huyo alikimbia kwenda kufunga mlango wa nje na kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani.
Hata hivyo, mtuhumiwa alifanikiwa kutoroka kwa kupanda juu ya dari na kutoboa ceiling board ya nyumba hiyo kabla ya kukimbia kusikojulikana.
Majirani walipofika kutoa msaada walimkuta marehemu amelala chini akiwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili, huku tayari akiwa amefariki dunia.
Kamanda Maigwa amesema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na mgogoro wa kifamilia uliotokana na tuhuma za ushirikina.
Amesema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.