WAZIRI MKUU AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI KATAVI

▪︎ Aagiza viongozi kushughulikia kero za wananchi badala ya kusubiri viongozi wakuu

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Machi 16, 2026 amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Katavi iliyoanza Machi 13, 2026 ambapo ameelekeza viongozi wa wilaya na halmashauri nchini kuhakikisha wanashughulikia changamoto za wananchi kwa wakati bila kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa.

Akizungumza na Viongozi hao katika kikao cha majumuisho kilichofanyika Ukumbi wa Katavi Social Hall, Manispaa ya Mpanda, Waziri Mkuu alisema mfumo wa ugatuaji wa madaraka unalenga kuwapa viongozi wa maeneo uwezo wa kutatua changamoto za wananchi katika ngazi zao.

 “Sio lengo la muundo wetu wa Serikali ugatuaji wa madaraka kwamba mambo yatatuliwe panapokuwa na ziara za viongozi wa kitaifa. Hoja zote tulizosikiliza zimeandikwa, nendeni mkazifuatilie moja baada ya nyingine na mzifikishe mwisho,” alisema.

Sekta ya Elimu

Katika sekta ya elimu, Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa viongozi wa Halmashauri ya Tanganyika kuhakikisha wanatatua changamoto zinazowakabili wanafunzi ikiwemo miundombinu ya shule na michango isiyo rasmi inayowakwamisha wanafunzi kupata elimu.

Ameagiza kufanyika kwa tathmini ya michango inayotozwa katika shule ili kuhakikisha wanafunzi hawazuiliwi masomo kwa sababu ya michango.

 “Ni jambo lisilokubalika mwanafunzi kukosa masomo kwa sababu ya michango, ilhali Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 35 kila mwezi kugharamia elimu bila ada,” alisema.

Aidha, aliwataka viongozi kufanya tathmini ya mahitaji ya elimu katika maeneo yao kwa kuzingatia kuwa kuanzia mwaka 2028 Serikali itaanza kutekeleza mfumo wa elimu ya lazima hadi kidato cha nne.

 “Kama elimu ya msingi ya lazima itakuwa hadi kidato cha nne, maana yake kila mtoto lazima afike kidato cha nne. Kwa lugha nyingine, kila kijiji kinapaswa kuwa na sekondari,” alisema.

Sekta ya Afya

Katika sekta ya afya, Waziri Mkuu aliagiza mkandarasi anayejenga jengo la huduma (Wing B) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi kuharakisha ujenzi wa mradi huo.

 “Fedha za mradi zipo na vifaa vimeshafika, hivyo mkandarasi aharakishe ujenzi ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisema.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha dawa zinazohitajika zinapatikana katika vituo vya afya na kuonya dhidi ya kuagiza dawa zisizohitajika.

 “Uagizaji wa dawa lazima uzingatie mahitaji. Tusiagize dawa ambazo hazitumiki zikaharibika huku fedha za Serikali zikiwa zimepotea,” alisema.

Sekta ya Maji

Kwa upande wa maji, Waziri Mkuu aliagiza wizara na taasisi zinazohusika kuhakikisha mradi wa maji uliokaguliwa unakamilika kwa wakati na wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi huo wanapata huduma ya maji.

Miundombinu ya Barabara

Katika sekta ya ujenzi na miundombinu, Waziri Mkuu aliagiza barabara zilizoharibika kutokana na mvua kushughulikiwa kwa dharura na kusisitiza kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya Kagwira – Karema.

Pia alielekeza barabara ya Kibaoni – Majimoto – Mlele kuingizwa katika mpango wa vipaumbele vya Serikali ili kuanza ujenzi mara tu taratibu za usanifu zitakapokamilika.

Nishati na Umeme

Katika sekta ya nishati, Waziri Mkuu alisema Serikali imefanikiwa kupeleka umeme katika vijiji 172 na vitongoji 534 kati ya 912 mkoani Katavi na kwamba kazi ya kupeleka umeme katika maeneo yaliyosalia inaendelea

Migogoro ya Ardhi

Waziri Mkuu pia aliagiza viongozi wa mkoa kufuatilia na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaosababisha migogoro ya ardhi kwa kuuza viwanja mara nyingi kwa watu tofauti.

 “Kuna watu wameuza kiwanja kimoja kwa watu watano. Hatuwezi kuangalia tu migogoro, lazima tujue chanzo chake na wahusika wachukuliwe hatua,” alisema.

Hitimisho la Ziara

Akihitimisha ziara hiyo, Waziri Mkuu aliwashukuru wananchi wa Katavi kwa ushirikiano wao na kuwataka viongozi wa mkoa kuhakikisha maelekezo yote yaliyotolewa yanatekelezwa kwa wakati.

 “Tumemaliza ziara ambayo imeleta matumaini kwa wananchi. Kilichobaki sasa ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa,” alisema.