Ufinyu wa bajeti unavyoathiri ujifunzaji sayansi kwa wanafunzi – 2

Rombo/Lushoto. Ufinyu wa bajeti umetajwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazochangia uhaba wa maabara za sayansi katika shule nyingi za sekondari za nchini.

Licha ya jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa muda mrefu, mgawo mdogo wa fedha katika sekta ya elimu umeendelea kuwa kikwazo katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya maabara.

Hali hiyo imeathiri zaidi shule za sekondari za Serikali zilizopo maeneo ya vijijini, ambazo nyingi hazina maabara za kisasa zenye vifaa vya kutosha kwa ajili ya kufundishia masomo ya fizikia, kemia na baiolojia.

Kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi hukosa fursa ya kujifunza kwa vitendo na hulazimika kusoma kwa nadharia pekee, jambo linalopunguza uelewa wao pamoja na uwezo wa kushindana katika masomo ya sayansi.

Walimu pia hulazimika kufundisha bila kufanya majaribio ya vitendo, hali inayopunguza ubunifu na motisha kwa wanafunzi wanaochagua masomo ya sayansi.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini baadhi ya maabara zimeishia katika hatua ya maboma kwa muda mrefu zikisubiri fedha za umaliziaji. Hali hiyo imejitokeza katika Wilaya ya Lushoto, ambako maabara kadhaa zilijengwa kwa nguvu za wananchi tangu mwaka 2018, lakini hadi sasa hazijakamilika kutokana na ukosefu wa fedha.

Kwa mujibu wa taarifa za halmashauri hiyo, kila mwaka hutengwa fedha kwa ajili ya kukamilisha maabara nne pekee, hali inayofanya shule nyingine kusubiri kwa muda mrefu kupata miundombinu hiyo muhimu.

Katika Wilaya ya Rombo, baadhi ya shule zimefikia hatua ya kubadili matumizi ya madarasa na kuyageuza kuwa maabara, ili kupunguza gharama za ujenzi wa majengo mapya.

Hata hivyo, hatua hiyo imeelezwa kuwa suluhisho la muda, kwani haikidhi kikamilifu mahitaji ya maabara za kisasa zinazotakiwa kwa ajili ya kufundishia sayansi.

Takwimu za bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha 2025/2026 zinaonesha Tanzania inahitaji kuongeza asilimia 40.68 ya maabara, ili kufikia kiwango kinachohitajika katika shule zote za sekondari za Serikali.

Kwa mujibu wa bajeti hiyo, katika mwaka wa fedha 2024/2025 kulikuwa na shule za sekondari 4,894 zilizohitaji maabara 14,682 ili kila shule iwe na maabara tatu za sayansi— kemia, baiolojia na fizikia. Hata hivyo, hadi kufikia mwaka huo kulikuwa na maabara 8,710 pekee, hali iliyosababisha upungufu wa maabara 5,972 nchini.

Wachambuzi wa elimu wanaeleza kuwa hali hiyo pia inachangiwa na changamoto za utekelezaji na usimamizi wa kanuni za usajili wa shule. Kwa mujibu wa Kanuni ya 15 (1)(c) ya Kanuni za Usajili wa Shule za Sekondari ya mwaka 2016, ofisa elimu wa mkoa au wilaya anatakiwa kuthibitisha uwepo wa maabara zinazofanya kazi kama sehemu ya tathmini ya mazingira ya shule kabla ya usajili wake kufanyika.

Akizungumza na Mwananchi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mraokeryo, Winled Kimario, anasema shule yake imeweka mpango wa kujenga maabara kupitia mipango ya maendeleo ya shule, lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa fedha.

“Wakati mwingine tunaweka kwenye mpango kazi kwamba tunahitaji maabara kwa sababu tulizonazo hazitoshelezi, lakini utekelezaji wake unakwama kwa sababu mahitaji ya shule ni mengi,” anasema.

Anafafanua kuwa mara nyingi shule hulazimika kuweka vipaumbele kwa kuzingatia mahitaji mengine muhimu, kama ujenzi wa jiko, ununuzi wa madawati na mahitaji mengine ya msingi.

“Unakuta mnahitaji jiko, viti au miundombinu mingine muhimu, hivyo inalazimu kuchagua kipi kipewe kipaumbele kwa wakati huo,” anasema.

Kwa upande wake, mwalimu wa Shule ya Sekondari Makiidi, John Venance, anasema changamoto nyingine inayochelewesha ujenzi wa maabara ni ufinyu wa maeneo katika baadhi ya shule.

Anasema katika baadhi ya shule, madarasa yaliyopo tayari yamechukua karibu eneo lote lililopo, hali inayofanya kuwa vigumu kupata nafasi ya kujenga maabara mpya.

“Madarasa yaliyopo yamemaliza eneo lote, hivyo wakati mwingine hata fedha zikapatikana bado inakuwa changamoto kujua maabara zitajengwa wapi,” anasema.

Hata hivyo, anaeleza kuwa iwapo kungekuwa na uamuzi wa dhati, baadhi ya majengo yangeweza kubomolewa na kujengwa majengo ya ghorofa ili kupanua matumizi ya eneo lililopo.

Mwalimu Venance anaiomba Serikali kuendelea kuunga mkono juhudi za kumaliza tatizo hilo na pia kuruhusu ushirikishwaji mkubwa wa wananchi, ili wachangie ujenzi wa maabara zinazohitajika shuleni.

Walimu na wadau wa elimu wanasema ukosefu wa maabara za sayansi katika shule nyingi za sekondari nchini unachangia wanafunzi wengi kukimbilia masomo ya sanaa na biashara badala ya sayansi.

Kwa mujibu wa walimu, kukosekana kwa miundombinu hiyo muhimu kunapunguza hamasa ya wanafunzi kuchagua masomo ya sayansi kwa sababu hawapati fursa ya kujifunza kwa vitendo.

Hali hiyo imefanya shule nyingi kushuhudia idadi ndogo ya wanafunzi wanaochagua mchepuo wa sayansi, huku wengi wakielekeza nguvu zao katika masomo ya sanaa na biashara.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Makiidi, John Venance, anasema wanafunzi wengi hukata tamaa kusoma sayansi kwa sababu mazingira ya kujifunzia hayaridhishi.

Anasema walimu wamekuwa wakijitahidi kuwashawishi wanafunzi kwa kuwaeleza umuhimu wa masomo ya sayansi na kuwapa motisha mbalimbali, lakini changamoto ya kukosekana kwa maabara inaendelea kupunguza mvuto wa masomo hayo.

“Tunawashawishi wanafunzi waone umuhimu wa masomo ya sayansi na kuwapa motisha, lakini tunaamini kwamba wanapopata nafasi ya kuingia maabara huvutiwa zaidi kwa sababu wanajifunza kwa kuona na kufanya majaribio tofauti na kusoma nadharia pekee,” anasema.

Katika Shule ya Sekondari Makiidi, wanafunzi 28 pekee ndio wanaosoma mchepuo wa sayansi kati ya wanafunzi 94 waliopo kidato cha nne.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mraokeryo, Winled Kimario, anasema ukosefu wa maabara wakati mwingine hulazimisha walimu kubeba vifaa vya majaribio na kwenda kufundishia katika madarasa ya kawaida.

Anasema hali hiyo si salama, kwa kuwa baadhi ya vifaa vya maabara vinahitaji uangalizi maalumu na vinaweza kuharibika au kuvunjika kwa urahisi.

Wadau waeleza athari zake

Akizungumzia hali hiyo, mdau wa elimu, Dk Luka Mkonongwa, anasema sayansi ni somo linalotegemea zaidi vitendo kuliko nadharia, hivyo kukosekana kwa maabara kunalifanya taifa kushindwa kuandaa wanasayansi halisi.

“Hakuna mwanasayansi anayeweza kutengenezwa kwa kutumia majaribio mbadala. Maabara ndiyo msingi wa sayansi. Tusitegemee kuingia katika ulimwengu wa sayansi kwa wanafunzi wanaofanya majaribio mbadala,” anasema Dk Mkonongwa.

Kwa upande wake, Dk Muhanyi Nkoronko, anasema kukosekana kwa maabara kunawafanya walimu kushindwa kufundisha mbinu na umahiri wa sayansi kwa ukamilifu.

Anasema hali hiyo inaweza kusababisha wanafunzi kupata maarifa yasiyo kamili katika masomo ya sayansi.

“Kukosekana kwa maabara kunawaathiri walimu na wanafunzi kwa pamoja. Walimu wanashindwa kufundisha ipasavyo, na wanafunzi wanakosa umahiri unaohitajika katika masomo ya sayansi,” anasema.

Anaonya kuwa hali hiyo inaweza kulifanya taifa kukosa wataalamu na wanasayansi wa kutosha katika siku zijazo, kwani maandalizi ya wataalamu hao yanapaswa kuanza tangu ngazi ya shule.

Wadau wanasema changamoto hiyo inaonekana pia katika udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu nchini, fani nyingi za sayansi hupokea wanafunzi wachache ikilinganishwa na fani za sanaa na biashara.

Takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) za mwaka 2024 zinaonesha kuwa katika mwaka wa masomo 2024/2025, fani za biashara, elimu, sayansi ya jamii na udaktari ndizo zilizoongoza kwa kudahili wanafunzi wengi zaidi vyuoni.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa mwelekeo huo umeendelea kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka wa masomo 2021/2022 hadi 2024/2025.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, kati ya wanafunzi 151,882 wa mwaka wa kwanza waliodahiliwa mwaka wa masomo 2024/2025 katika ngazi mbalimbali za elimu ya juu, jumla ya wanafunzi 106,249 walichagua kusoma fani hizo.

Katika kipindi hicho cha miaka minne, fani ya biashara imeonesha ukuaji mkubwa wa udahili kwa asilimia 42.35, ikifuatiwa na sayansi ya jamii iliyokua kwa asilimia 21.4, elimu asilimia 18.14 na udaktari pamoja na sayansi za tiba kwa asilimia 10.71.

Hata hivyo, udahili katika fani ya ualimu ulipungua kwa asilimia 16.42 kati ya mwaka wa masomo 2023/2024 na 2024/2025.

Kwa upande wa fani za sayansi maalumu, takwimu zinaonesha kuwa madini na sayansi ya dunia ndizo fani zinazodahili wanafunzi wachache zaidi katika vyuo vikuu kwa miaka minne mfululizo.

Katika mwaka wa masomo 2024/2025, wanafunzi 604 pekee ndio walidahiliwa kusoma fani ya madini na sayansi ya dunia, ikiwa ni ongezeko kidogo kutoka wanafunzi 570 waliokuwapo mwaka 2021/2022.

Hata hivyo, idadi hiyo ilishuka hadi wanafunzi 421 mwaka wa masomo 2022/2023 kabla ya kuongezeka tena na kufikia wanafunzi 589 mwaka 2023/2024.

Licha ya ongezeko hilo la takribani asilimia sita katika kipindi cha miaka minne, wadau wa elimu wanasema fani hiyo bado inaendelea kushuhudia udahili mdogo, hali inayochangiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa msingi imara wa elimu ya sayansi katika ngazi za chini za elimu.

Kwa nini shule binafsi hakuna uhaba

Wakati ukata ukizitesa shule za Serikali, kwa shule binafsi ni tofauti. Kabla ya kupewa usajili, ni lazima ziwe na miundombinu inayotakiwa.

Ikiwa kitakosekana kitu chochote, shule hiyo haipaswi kupewa usajili kutokana na kilichobainishwa kwenye mwongozo wa usajili.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (Tamongosco), Benjamin Nkonya, anasema mfumo wa udhibiti wa ubora bado ni tatizo na unatoa upendeleo kwa Serikali.

Hiyo ni kwa sababu wanaotakiwa kuzuia shule isisajiliwe bila ya kuwa na miundombinu, ni waajiriwa wa Serikali, hivyo inakuwa ngumu kumaliza tatizo hilo.

“Mfumo wa ugharamiaji nao ni sababu, kwa shule za Serikali, wanafunzi wanapelekwa tu, ile inayogharamiwa ni Serikali. Kila kitu kwenye shule binafsi mzazi anaangalia kwanza ubora wa shule, ndiyo analeta mtoto. Kusipokuwa na ubora wa elimu, anapeleka katika shule nyingine. Moja ya kinachowezesha wanafunzi wafaulu ni maabara. Tunawekeza sana kwa sababu ikikosekana hakutakuwa na ufaulu mzuri,” anasema.

Nini wanafanya kuvutia wanafunzi

Ili kuvuta wanafunzi wengi kusoma masomo hayo, walimu wamekuwa wakitoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wanaofanya vizuri, ikiwemo madaftari, fedha au kuwatangaza mbele ya wenzao.

Mwalimu wa fizikia kutoka Shule ya Sekondari Shambalai, Deusdedith Mkama, anasema kutengeneza mazingira rafiki kwa wanafunzi ni mojawapo ya mbinu zinazotumika kufanya wanafunzi wapende somo hilo.

“Moja ya motisha tunayotumia ni kumsifia mtoto akifanya vizuri mbele ya wenzake. Pia tuna medali ambayo huwa tunaitoa kwa mwanafunzi, yule anayefanya vizuri anakuwa anaishikilia kwa wakati huo hadi apatikane atakayefanya vizuri zaidi. Hii inaongeza ari ya wanafunzi na ushindani,” anasema.

Kauli yake inaungwa mkono na Mwalimu Godson Mshana, anasema motisha ndiyo mbinu pekee inayotumika kuvutia wengine.

“Unajua, unapomtangaza mtoto mbele ya wanafunzi wenzake unamuongezea ari ya kujituma na kufanya vizuri zaidi katika masomo yake,” anasema.

Akijibu namna wanavyoboresha miundombinu katika shule zilizo na ufinyu wa maeneo, Naibu Waziri wa Tamisemi, Reuben Kwagilwa, anasema maeneo ambayo yanakua kwa kasi na kushuhudia ongezeko la watu yamekuwa yakikabiliana na suala hilo.

Hilo limeshuhudiwa zaidi katika baadhi ya miji mikubwa, ikiwemo Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

Alitolea mfano wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, ambapo kwa siku moja takribani watoto 130 huzaliwa. Anasema ili kuendana na kasi hiyo na kupunguza ufinyu wa miundombinu ya shule, unalazimika kujenga madarasa matatu kila siku.

Lakini kutokana na kutambua hilo, sasa wamebadili mfumo wa ujenzi wa shule katika miji inayokua, kutoka majengo mtawanyo hadi shule za ghorofa, ili kupata madarasa ya kutosha, ofisi za walimu na maabara.

“Ukienda Dar es Salaam sasa hivi, hatujengi tena majengo mtawanyo, bali maghorofa. Ukienda shule nyingine unakuta tumelazimika kuvunja kabisa majengo ya awali ,ili tujenge majengo mapya ya kwenda juu,” anasema.

Kutokana na kuendelea kuwapo kwa mahitaji ya uboreshaji miundombinu, Serikali imekuwa ikiendelea kutenga fedha kila mwaka.

Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ya mwaka 2025/2026, Serikali imepanga kufanya umaliziaji wa maboma ya maabara 350 pamoja na ununuzi wa vifaa na kemikali za maabara katika shule mpya 300 za sekondari.

Hilo linakwenda kufanyika wakati ambapo Serikali ilikuwa imenunua na kusambaza kemikali za maabara katika shule za sekondari za kata 231, na vifaa vya maabara kwa shule 486 vilivyonunuliwa katika awamu mbili.

“Vifaa vya awamu ya kwanza vilisambazwa katika shule 231, zikiwemo shule nane kati ya 26 za mikoa za wasichana. Vifaa vya maabara na kemikali kwa awamu ya pili, kwa ajili ya shule 255 zilizobaki, vinatarajiwa kupokelewa na kusambazwa kabla ya tarehe Juni 30, 2025,” ilieleza bajeti hiyo.

UTILITY: Fedha zilizotengwa

Wakati ufinyu wa bajeti ukitajwa kuwa moja ya sababu, katika miaka minne mfululizo Serikali ilikuwa ikitenga kiwango cha fedha kwa ajili ya umaliziaji wa maabara nchini au kuweka lengo la kununua vifaa mbalimbali na kemikali.

Hayo yalibainishwa kupitia hotuba za bajeti za Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa za kati, kutoka mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2025/2026.

Katika bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali iliahidi kutoa Sh8.73 bilioni kwa ajili ya umaliziaji wa vyumba 291 vya maabara katika shule mbalimbali za sekondari nchini, na hadi Februari 23, mwaka 2023, Sh8.13 bilioni zilikuwa zimepokelewa kwa ajili ya kufanya umaliziaji wa vyumba 217.

Baada ya kufanyika kwa umaliziaji mwaka 2023/2024, Serikali ilipanga kununua vifaa vya maabara na kemikali kwa ajili ya shule mpya 234 za sekondari za kata zilizokuwa zimejengwa katika halmashauri mbalimbali nchini bila kuainisha kiwango cha fedha ambacho kingetumika.

Mwaka 2024/2025, pia hakikutajwa kiwango cha fedha ambacho kingetumika, lakini Serikali ilipanga kumalizia maabara za masomo ya sayansi 203 za sekondari.

Hiyo iliendelea hadi mwaka 2025/2026, ambapo bajeti hii ilibainisha kuwa Sh10.5 bilioni zilitengwa kwa ajili ya umaliziaji wa maabara zilizojengwa kwa nguvu za wananchi katika halmashauri mbalimbali nchini.