Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Pope Leo, anatarajiwa kuanza ziara rasmi katika mataifa manne ya Afrika kuanzia Aprili 13 hadi 23, 2026, ikiwa ni safari yake ya tatu ya kitume nje ya Italia tangu aanze uongozi wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Holy See Press Office, Papa Leo atatembelea mataifa ya Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea katika safari ya siku 11 itakayohusisha hotuba 10, mahubiri nane na salamu sita katika miji 11.
Ziara hiyo inafuatia safari yake ya mwaka 2025 katika Mashariki ya Kati alipokwenda Uturuki na Lebanon, huku safari nyingine ya Ulaya ikitarajiwa kufanyika Machi 28 mwaka huu katika Monaco.
Ratiba inaonyesha Papa Leo ataanza ziara yake katika Algeria, ambapo anatarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Algiers Aprili 13.
Mara baada ya kuwasili, kiongozi huyo atatembelea Maqam Echahid Martyr’s Memorial, kumbukumbu ya mashujaa wa vita vya uhuru wa Algeria iliyoanzishwa mwaka 1982 kuadhimisha miaka 20 ya uhuru wa taifa hilo, ambako atatoa salamu kwa wananchi.
Baadaye ataelekea katika Ikulu ya Rais kukutana na Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, kabla ya kutoa hotuba kwa viongozi wa serikali, wawakilishi wa asasi za kiraia na wanadiplomasia katika Kituo cha Mikutano cha Djamaa el Djazair Conference Center.
Katika siku hiyo pia, Papa Leo atatembelea Great Mosque of Algiers, moja ya misikiti mikubwa duniani inayoweza kuchukua hadi waumini 120,000.
Baadaye atafanya ziara ya faragha katika Kituo cha Welcome and Friendship kinachoendeshwa na masista wa Augustinian Missionary Sisters katika mji wa Bab El Oued.
Papa Leo atahitimisha siku hiyo kwa kutoa hotuba kwa jamii ya Algeria katika Basilica of Our Lady of Africa.
Siku ya pili ya ziara hiyo, Aprili 14, Papa Leo atasafiri kwa ndege kwenda mji wa bandari wa Annaba, uliokua kutoka mji wa kale wa Hippo Regius, uliowahi kuwa makazi ya mtakatifu Saint Augustine of Hippo.
Akiwa huko, atatembelea eneo la kihistoria la Hippo pamoja na nyumba ya wazee inayoendeshwa na Little Sisters of the Poor, ambapo atasalimia wakazi na wafanyakazi.
Baadaye Papa Leo atafanya mkutano wa faragha na wanachama wa Order of Saint Augustine katika nyumba ya jumuiya ya Waagostino kabla ya kuongoza ibada ya Misa katika Basilica of St. Augustine.
Pia, atarejea kwa ndege mjini Algiers kuendelea na ratiba ya safari yake ya kitume barani Afrika.
Endelea kufuatilia Mwananchi
