Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Elsie Kanza, ametajwa miongoni mwa viongozi 100 wenye ushawishi barani Afrika, akiungana na majina makubwa kutoka kwenye siasa, biashara, michezo na taasisi za kimataifa.
Kutajwa kwa Kanza kunaakisi kuongezeka kwa ushawishi wake katika diplomasia ya kimataifa, hususan jijini Washington ambako amekuwa sauti muhimu katika kuwasilisha maslahi ya Afrika kwa lugha ya sera inayoeleweka katika Marekani.
Katika orodha hiyo, Kanza ameungana na viongozi mashuhuri kama Ngozi Okonjo-Iweala, Mkurugenzi Mkuu wa World Trade Organization; Rais wa Kenya, William Ruto; pamoja na Rais wa Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Elsie Kanza.
Wengine ni pamoja na Ibrahim Traoré, Rais wa Burkina Faso; Rais wa Angola João Lourenço, ambaye pia ni Mwenyekiti wa African Union; na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.
Katika sekta ya michezo na burudani, orodha hiyo imetambua mafanikio ya wanariadha wa Kenya, Faith Kipyegon na Beatrice Chebet, pamoja na msanii wa Afrika Kusini Tyla, wanaoendelea kuitangaza Afrika kimataifa.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, nguvu ya Kanza ipo zaidi katika diplomasia makini inayojengwa juu ya uaminifu, mahusiano na uwazi wa kimkakati kuliko kuonekana hadharani. Ametajwa kuwa mmoja wa viongozi wanaochangia kubadili simulizi ya Afrika kutoka bara linalotegemea misaada hadi kuwa kitovu cha uwekezaji na uchumi duniani.
Akiwa na historia ya uchumi na uzoefu wake kama Mkuu wa Kanda ya Afrika katika World Economic Forum, Kanza amejiweka katika nafasi ya kipekee inayounganisha serikali, masoko na taasisi za kimataifa hali inayoongeza ufanisi wake katika diplomasia.
Rais wa Kenya, William Ruto. Picha na Mtandao
Ripoti hiyo inanukuu kuwa: “Anaizungumza Afrika kwa uhalisia wa kiuchumi na uelewa wa kiutawala, akisisitiza bara hili kama mshirika wa kimkakati katika masuala ya uwekezaji, siyo tu eneo la misaada na migogoro.”
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaeleza kuwa jijini Washington, ambako ushawishi hujengwa kupitia uaminifu na mahusiano, Kanza ameonyesha umahiri kwa kutumia mbinu ya nidhamu na umakini, akitanguliza hoja zenye uzito badala ya kelele.
Msanii wa Afrika Kusini, Tyla
Aidha, ametajwa kuwakilisha kizazi kipya cha uongozi wa Afrika kinachosisitiza uhuru wa maamuzi, uthabiti wa kiuchumi na nafasi ya bara hilo katika kushughulikia changamoto za dunia kama mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na nishati.
Kupitia kazi yake, Kanza anaonekana kuendeleza mabadiliko mapya ya namna Afrika inavyojenga ushawishi wake kimataifa kutoka katika mifumo ya zamani ya nguvu hadi mtazamo wa kimkakati, unaolenga matokeo na unaotumia mtandao mpana wa ushirikiano.
