MSHAMBULIAJI wa Yanga Laurindo Dilson ‘Depu’ amechaguliwa kuwa mchezaji Bora wa mwezi Februari wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa mwaka 2025/26, huku kocha wa Simba, Steve Barker akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa ligi hiyo kwa mwezi huo.
Katika taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi, imesema:
Laurindo alionesha kiwango kizuri chenye mwendelezo kwa mwezi huo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao mawili katika michezo miwili ambayo Young Africans ilicheza na kuisaidia timu yake kusalia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Mshambuliaji huyo aliwashinda beki Rushine De Reuck wa Simba na kiungo Idd Selemani ‘Nado’ wa Azam alioingia nao fainali katika mchakato wa Tuzo za Mwezi uliofanywa na Kamati ya Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Steve Barker aliyeingia fainali na Pedro Goncalves wa Young Africans na Florent Ibenge wa Azam aliiongoza timu yake kushinda michezo miwili na kutoka sare moja hivyo kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Wakati huohuo Meneja wa Uwanja wa Isamuhyo, Said Mpuche, amechaguliwa kuwa Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi Februari kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo pamoja na masuala yanayohusu miundombinu uwanjani.
Katika hatua nyingine Ramadhan Karanje wa B19 amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwezi Februari wa Ligi ya NBC Championship 2025/26, huku Mbwana Makata wa Polisi Tanzania akichaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi huo.
Karanje aliyeingia fainali na Obrey Chirwa wa Kagera Sugar na Tariq Seif wa Polisi Tanzania, alionesha kiwango chenye mwendelezo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao manne (4) kwa dakika 404 za michezo mitano aliyocheza.
Kwa upande wa Makata aliyeingia fainali na Juma Kaseja wa Kagera Sugar na Zuberi Katwila wa Geita Gold, aliiwezesha timu yake kushinda michezo minne na kutoka sare mmoja hivyo kupanda kutoka nafasi ya sita hadi ya tano kwenye msimamo wa Ligi ya NBC Championship.