Mpango asimulia Magufuli alivyomsisitiza kumtegemea Mungu, kudhibiti mapato ya Serikali

Dar es Salaam. Katika kumbukumbu zake kuhusu aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango anasimulia kwa sauti ya utulivu lakini yenye hisia akikumbuka kiongozi aliyemfundisha kumtegemea Mungu na kusimamia fedha za umma kwa nidhamu isiyoyumba.

Dk Mpango ametoa simulizi hiyo leo Chato inakofanyika misa takatifu ya kumbukumbu ya miaka mitano ya kifo cha Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Akirejea nyakati walizofanya kazi pamoja, Dk Mpango amesema moja ya mambo yaliyomgusa zaidi kwa hayati Magufuli ni namna alivyoweka imani kwa Mungu kuwa sehemu ya maisha na uongozi.

Amesimulia kuwa wakati fulani alipokuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo, alimweleza Magufuli kuhusu hali hiyo.

Badala ya kumpa ushauri wa kawaida tu, Rais huyo wa zamani alimpatia zawadi ya kitabu cha maombi ya Rozari (mawaridi) na hata kuwatafuta masista kutoka Karagwe ili wamuombee.

Kwa Dk Mpango amesema tukio hilo lilikuwa ishara ya namna kiongozi huyo alivyoamini nguvu ya maombi.

Simulizi hiyo halikuishia hapo, amesema wakati alipokuwa akiugua, Magufuli aliendelea kuonyesha upendo wa karibu wa kifamilia, hata kumshirikisha mkewe, Janeth Magufuli, katika kumuombea.

“Alimuita  mama Janeth aniombee kwenye simu. Unaona ni jinsi gani alikuwa karibu na Mungu haya ni mafunzo makubwa.”

Mbali na masuala ya kiroho, Dk Mpango anakumbuka pia safari yake ya uongozi chini ya Magufuli iliyoanza kwa kuaminiwa kushika nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kabla ya baadaye kuteuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Amesema Magufuli alimweleza wazi kuwa nafasi hiyo haikuwa ya kawaida, bali ni dhamana aliyokabidhiwa na Mungu, hivyo alipaswa kuitumikia kwa uadilifu na bidii kubwa.

Katika mazungumzo yao ya mwanzo kabisa, Dk Mpango anakumbuka alipewa jukumu moja kuu la kuhakikisha mapato ya Serikali yanaongezeka.

Chini ya uongozi wa Magufuli, amesema, juhudi kubwa zilifanyika kuboresha ukusanyaji wa kodi.

“Nilipoingia tulikuwa tunakusanya takribani Sh850 bilioni kwa mwezi, lakini ndani ya muda mfupi tukafikisha hadi Sh1.3 trilioni,” amesema.

Amefafanua kuwa hata hivyo, kwa Magufuli, kuongeza mapato pekee hakukutosha. Nidhamu katika matumizi ya fedha za umma ilikuwa muhimu zaidi.

Dk Mpango anakumbuka tukio moja lililomfundisha somo hilo kwa vitendo.

“Kulikuwa na orodha ndefu ya viongozi waliokuwa wamepangwa kusafiri nje ya nchi. Kwa kuwa gharama zilionekana kuwa kubwa, aliona ni busara kwanza kupata mwongozo wa Rais.

Amesema Magufuli alipoiangalia orodha hiyo, aliikata kuanzia tarehe za safari hadi idadi ya watu waliokuwa wanafuatana na viongozi hao.

“Aliniambia sasa nimekuonesha mfano. Umefanya vizuri kukusanya mapato, lakini usije kuyagawanya hovyo,”.

Amesema Magufuli alikuwa akisisitiza  mara kwa mara kuwa fedha za Serikali lazima zielekezwe katika maeneo yanayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.