Dar es Salaam. Moto ambao chanzo chake bado hakijajulikana unaendelea kuwaka katika kiwanda kinachojishughulisha na uzalishaji wa nywele bandia, maarufu rasta kilichopo eneo la Buguruni Sukita, Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mashuhuda moto huo umeanza usiku wa kuamkia leo Jumanne, Machi 17, 2026 na kuzua taharuki kwa wafanyakazi na watu wanaoishi jirani na kiwanda hicho.
Pia moto huo umeleta uharibifu wa baadhi ya mali zilizokuwa ndani ya kiwanda hicho.
Mwananchi imefika eneo hilo saa 2:30 asubuhi na kushuhudia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiendelea kuuzima moto huo.
Hata hivyo hadi kufika saa 6:00 mchana bado moto huo umeendelea kuwaka huku juhudi za kuudhibiti zikiendelea.
Mwananchi pia imeshuhudia watu wakiwa wamekaa kwa makundi wakishuhudia tukio hilo, huku baadhi wakiwamo waliojitambulisha kama wafanyakazi wa kiwanda hicho wakiwa katika nyuso za huzuni.
Wengine wakiangusha kilio kwa hofu ya kupoteza ajira wanayoitegemea kukidhi mahitaji yao ya kila siku.
Askali wa kikosi cha zimamoto wakipambana kuzima moto uliowaka katika kiwanda cha rasta, kilichopo Sukita jijini Dar es Salaam leo Machi 17, 2026. Picha na Michael Matemanga
Tayari viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ilala akiwemo Mkuu wa Wilaya, Edward Mpogolo wamefika katika eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa mashuhuda ambaye anafanya kazi katika kiwanda hicho, Victoria Chuma amesema alipokea simu saa nane usiku kutoka kwa mfanyakazi mwenzie kuwa kiwanda kinawaka moto.
Victoria ambaye ni mkazi wa Kigogo amesema alijiandaa kwa haraka na kufika katika kiwanda hicho anachofanyia kazi na kushuhudia moto ukiendelea kuwaka huku juhudi za kuuzima zikiendelea.
Askali wa kikosi cha zimamoto wakipambana kuzima moto uliowaka katika kiwanda cha rasta, kilichopo Sukita jijini Dar es Salaam leo Machi 17, 2026. Picha na Michael Matemanga
“Hapa nilipo nimechanganyikiwa sijui nitaishije, ninapopatarajia kupata kipato pameteketea,” amesema Victoria.
Naye Abdallah Athuman amesema yupo eneo hilo tangu alfajiri ambapo alikuta moto huo ukiwa umeteketeza eneo kubwa la kiwanda.
