Pigo lingine kwa Serikali ya Tanzania

Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imeiamuru Serikali ya Tanzania kwamba, ndani ya miezi 24 iwe imezifanyia marekebisho Katiba yake na ya Zanzibar katika ibara zinazokiuka mikataba ya kimataifa.

Ibara hizo ni Ibara ya 74(12) ya Katiba ya Tanzania na Ibara ya 119(13) ya Katiba ya Zanzibar zinazozuia Mahakama kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa ya Katiba hizo.

Huu unakuwa uamuzi wa pili mzito kutolewa na Mahakama hiyo ndani ya wiki mbili, baada ya Machi 6, 2026 kuiamuru Serikali ndani ya miezi 24, kurekebisha kifungu cha Katiba ya Tanzania kinachozuia matokeo ya Rais kuhojiwa kortini.

Ibara ya 41(7) ya Katiba ya Tanzania, inasema iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais, basi hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.

Hukumu hiyo mpya imetolewa Machi 6,2026 na Jopo la majaji 10 wa Mahakama hiyo kufuatia maombi namba 040/2020 na 043/2020 yaliyofunguliwa na Abdul Nondo, Deusdedit Rweyemam na Paul Kaunda, ambayo mahakama iliyaunganisha.

Nondo na wenzake walifungua maombi hayo dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku yakigusa pia Katiba ya Zanzibar ya 2010.

Majaji waliotoa hukumu hiyo ni Rais wa Mahakama hiyo, Blaise Tchikaya na majaji Chafika Bensaoula, Rafaa Ben Achour, Suzanne Mengue, Tujilane Chizumila, Stella Anukam, Dumisa Ntsebeza, Modibo Sacko, Dennis Adjei na Duncan Gaswaga.

Mahakama imebaini ibara hizo mbili zinakiuka Kifungu 3(2) cha Mkataba wa Afrika kwani vinaondoa mamlaka ya Mahakama kwa watu binafsi wanaotaka kupinga hatua za Tume Huru ya Taifa yaUchaguzi  (INEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Zimeamriwa kuchukua hatua zote muhimu za Kikatiba na za kisheria, ndani ya miezi 24 tangu kutolewa kwa hukumu, ili kuhakikisha ibara hizo zinafanyiwa marekebisho ili kuondoa ukiukaji wa Ibara ya 3(2) na 7(1)(a) ya Mkataba huo.

Pia, Serikali hizo mbili zimeamriwa kuwasilisha kwa Mahakama hiyo, ndani ya miezi 12, ripoti kuhusu hali ya utekelezaji wa uamuzi huo na baada ya hapo, kila baada ya miezi sita mpaka Mahakama itakapoona utekelezaji kamili umefanyika.

Mahakama imeamuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchapisha Hukumu hii ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia ilipotolewa, kwenye tovuti za Mahakama na Wizara ya Katiba na Sheria na ibakie humo kwa mwaka mmoja.

Maombi ya Nondo na wenzake

Katika maombi yake, Nondo na wenzake ambao walitetewa na mawakili Jebra Kambole na Prisca Chogero, walifungua maombi hayo wakipinga ibara mbalimbali za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na ya Zanzibar ya 2010.

Nondo alieleza Ibara za 74(1), 74(3), 74(5) na 74(14) zinakiuka Mkataba wa Afrika Kuhusu Haki za Binadamu, mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu (UDHR) na Mkataba Kimataifa wa Haki za kiraia na kisiasa (ICCPR).

Kwa mujibu wa mleta maombi huyo wa kwanza, alidai kuwa ibara hizo za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilikuwa zinakiuka ibara ya 1,3 na 13(1) ya Mkataba huo wa Afrika na ibara ya 21 ya UDHR na Ibara ya 25(a) na (b) ya ICCPR.

Nondo alidai kuwa ibara ya 74(1) ya Katiba inayoanzisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) sasa INEC, ilitoa muundo wa wajumbe wa tume hiyo ambao wanateuliwa na Rais wa Tanzania.

Aliendelea kudai kuwa, ibara hiyo inatoa mamlaka kamili na yasiyozuiliwa kwa Rais kuteua wajumbe wa tume ya uchaguzi bila kinga yoyote, jambo linalokiuka mikataba hiyo inayotoa usawa mbele ya sheria na uchaguzi huru na haki.

Pia, alipinga ibara zingine ikiwamo ya 74(5) inayompa Rais mamlaka ya kumuondoa mjumbe yeyote wa tume ya uchaguzi na kukiuka mikataba hiyo ya kimataifa inayotaka hakikisho la ajira (security of tenure) kwa wajumbe wa tume.

Nondo alidai pia kuwa, ibara ya 74(14) ya Katiba kinachopiga marufuku watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa inakiuka ibara ya 1,3 na 13(1) ya mkataba huo wa Afrika pamoja na mikataba ya UDHR na ICCPR.

Kwa upande wao, mleta maombi wa pili Deusdedit Rweyemam na wa tatu, Paul Kaunda, wao walidai kuwa, ibara ya 74(1) na 74(12) ya Katiba ya Tanzania na Ibara ya 119(13) ya Katiba ya Zanzibar inakiuka mikataba hiyo mitatu nchi iliyoridhia.

Ibara hizo, ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zinasema hakuna Mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katika kutekeleza madaraka yake.

Walisisitiza kuwa, vifungu vya Katiba vilivyotajwa vinawanyima watu fursa ya kupata haki (suluhu za kisheria) kiholela na bila sababu za msingi, huku kwa wakati huo huo vikizuia jukumu la Mahakama katika utoaji wa haki hapa nchini.

Serikali kwa upande wake, ambayo iliwakilishwa Dk Ally Possi ambaye ni wakili mkuu wa Serikali, ilipinga maombi hayo ikisema Mahakama hiyo haikuwa na mamlaka (jurisdiction) ya kusikiliza maombi hayo ya Nondo na wenzake.

Katika pingamizi lingine, Serikali iliiomba Mahakama ione kuwa maombi hayajatimiza masharti ya kukubalika yaliyowekwa katika kifungu cha 56(6) cha Mkataba ikisomwa pamoja na kanuni ya 50(2)(f) ya kanuni za Mahakama hiyo.

Hata hivyo, mapingamizi hayo yalikataliwa na mahakama ikasema inayo mamlaka ya kusikiliza na kuamua juu ya maombi hayo na shauri hilo kusikilizwa.

Katika majibu yake, Serikali iliomba mahakama itamke kuwa Ibara ya 74(1),74(3),74(5) na 74(14) za Katiba hazikiuki mikataba ya kimataifa iliyotajwa, hivyo iimpe nafuu itakayoona inafaa na kutupa maombi hayo kwa gharama.

Kuhusu ibara ya 74(1 na 74(12) ya Katiba ya Tanzania na Ibara 119 (13) ya Katiba ya Zanzibar, Serikali ilisema ibara hizo hazikiuki mikataba hiyo ya kimataifa.

Baada ya kusikiliza mawasilisho ya pande mbili, jopo la majaji hao 10 lilikubaliana na hoja za waleta maombi kuwa ibara ya 74(12) ya Katiba ya Tanzania na Ibara 119(13) ya Katiba ya Zanzibar zinakiuka ibara ya 3(2) ya Mkataba wa Afrika.

Hiyo ni kwa sababu ibara hizo zinazuia wananchi ambao wanania ya kupinga matendo yaliyofanywa na NEC (sasa INEC) na ZEC kwa upande wa Zanzibar.

“Mahakama Inabaini Serikali ya Tanzania imekiuka kifungu cha 7(1)(a) cha Mkataba wa Afrika kwa kiasi ambacho kifungu cha 74(12) cha Katiba yake na kifungu cha 119(13) cha Katiba ya Zanzibar vinaondoa mamlaka ya Mahakama kwa watu binafsi wanaotaka kupinga hatua za NEC na ZEC,”walisema majaji hao.

Hata hivyo, majaji hao waliyakataa maombi mengine ya vifungu vingine vya Katiba vilivyokuwa vinalalamikiwa hasa vile alivyoorodhesha Nondo.

Mahakama pia ilikataa ombi la waleta maombi la kutaka Serikali ianzishe kampeni ya elimu ya uraia ili kutoa ufahamu kwa umma juu ya athari za hukumu ya mahakama hiyo ambayo Tanzania imeridhia kuanzishwa kwake.

Mbali na hilo, Mahakama imeiamuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurekebisha ibara ya 74(12) ya Katiba ya Tanzania na Ibara ya 119(13) ya Katiba ya Zanzibar, marekebisho hayo yafanyike ndani ya miezi 24.