MHE. MCHENGERWA ATOA WITO KWA WATANZANIA KUTUMIA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI KUIMARISHA UMOJA WA KITAIFA

-Aendelea kufuturisha, Mwaseni na Kipugila

-Wananchi washiriki futari, waipongeza Serikali kwa maendeleo

Na Yohana Kidaga- Mkongo

Mbunge wa Rufiji na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa waislamu na watanzania wote kwa ujumla kuendeleza dua, amani na mshikamano katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, akisisitiza kuwa kipindi hiki ni cha toba, kujisafisha na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Akizungumza kwenye eneo la Mkongo kata ya Mwaseni wilayani Rufiji, Machi 16,2026 ambapo aliendelea kufuturisha wananchi wa kata ya Mwaseni na Kipugila ikiwa ni mwendelezo baada ya kufuturisha wananchi wa za Utete, Chemchem,Mohoro, Chumbi,Mbwala na Shela kuanzia Machi14, mwaka huu, Mhe. Mchengerwa alisema matukio haya ya futari yatumike kuwaunganisha wananchi na Mwenyezi Mungu pia na wao wenyewe ili kuongeza umoja na mshikamano.

Alisema Ramadhani ni zaidi ya kujizuia kula na kunywa, bali ni safari ya kurekebisha nafsi na kuimarisha maadili katika jamii.

“Tunapaswa kuitumia Ramadhani kama darasa la kujitathimini, kuimarisha udugu na kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie rehema na amani katika taifa letu”. Alisisitiza Waziri Mchengerwa.

Wananchi wa kata wamemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa upendo wake wa kuendelea kutoa futari miaka minne mfululizo katika jimbo hilo na kusema kitendo hicho siyo tu kitendo cha imani bali ni funzo kubwa la upendo baina yake na wananchi wake na kumwomba kuendelea kufanya hivyo kila anapojaaliwa kufanya hivyo.

“Sisi wananchi tunaendelea kujifunza mengi kutoka kwa Mbunge wetu, kwamba kupitia futari amekuwa akituunganisha na kutuweka pamoja, hii inakuza umoja na udugu wetu”. Alisema Bi. Fatuma Said Mkazi wa Mkongo