Mbeya. Wakati baadhi ya wakulima wilayani Kyela mkoani Mbeya wakitishia kukata na kung’oa miti ya kakao kutokana na anguko la bei, Chama Kikuu cha Ushirika Kyela (Kyecu) kimewataka kuwa wavumilivu huku kikitoa matumaini ya kurejea kwa bei nzuri ya zao hilo.
Kwa takribani miaka miwili iliyopita, bei ya kakao ilikuwa ikifikia hadi Sh32,000 kwa kilo moja, lakini ndani ya mwezi mmoja uliopita iliporomoka hadi Sh5,440. Hata hivyo, katika mnada wa wiki hii bei imepanda kidogo na kufikia Sh6,400, huku bei elekezi ya Serikali ikiwa Sh10,000 kwa kilo.
Kutokana na kushuka kwa bei hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra) iliitisha kikao jijini Mbeya, kikihusisha wadau kutoka mikoa minne inayolima zao hilo, kwa lengo la kujadili sababu za anguko hilo na kuweka mikakati ya kulikabili.
Mkulima Abel Mwambone amesema wakulima wengi wameathirika kiuchumi na baadhi yao wanafikiria kufyeka mashamba ya kakao na kupanda migomba, wakiamini zao hilo halina faida tena. Ameongeza kuwa si mara ya kwanza kwa wakulima kufanya hivyo, kwani hata zamani walilazimika kukata mikorosho kutokana na magonjwa na kuhamia kakao.
“Bei imetuchanganya sana. Tukiuliza tunaambiwa ni soko la dunia. Wakulima wengi wamekata tamaa, ingawa binafsi bado nawatia moyo tuwe watulivu kwa matumaini hali itabadilika,” amesema Mwambone.
Naye mkazi wa kijiji cha Kyela Ndandalo, Isaya Mwakimo amesema licha ya changamoto ya bei, Kyecu imekuwa karibu na wakulima kwa kuwapa hamasa ya kuendelea kulima. Ameeleza kuwa suluhisho la kudumu ni kuwa na kiwanda cha kuchakata kakao wilayani humo ili kuongeza thamani ya zao hilo.
“Tunahitaji kuwa na kiwanda chetu Kyela ili tuweze kuchakata na kuuza wenyewe ndani na nje ya nchi badala ya kusubiri wanunuzi wa nje,” amesema Mwakimo.
Akizungumzia mikakati iliyopo, Meneja Mkuu wa Kyecu, Aman Hankungwe amesema kushuka kwa bei kunatokana na uzalishaji mkubwa katika soko la dunia, hasa kutoka nchi za Afrika Magharibi.
Amesema wakulima wanapaswa kuendelea kuzalisha kwa wingi na ubora, akisisitiza kuwa kakao ya Kyela ni ya asili (organic) na ina soko zuri. Pia ameongeza kuwa Kyecu inapanga kujenga kiwanda cha kuchakata zao hilo pamoja na kutoa miche zaidi ya 100,000 kila mwaka ili kuongeza uzalishaji.
“Tumeanza kuona dalili za bei kupanda kutoka Sh5,440 hadi Sh6,400. Tunatarajia ndani ya miaka mitano uzalishaji uongezeke kutoka tani 11,000 za sasa hadi kufikia tani 15,000,” amesema Hankungwe.