Nchimbi: Magufuli ameacha darasa la uongozi

Dar es Salaam/Chato. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amesema maisha na uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli yalikuwa darasa muhimu kwa viongozi na Watanzania kwa ujumla, akisisitiza kuwa namna bora ya kumuenzi ni kuishi na kutenda yale aliyoyaamini.

Nchimbi ameyasema hayo leo Machi 17, 2026 alipozungumza baada ya misa takatifu ya kumbukizi za miaka mitano tangu kifo cha kiongozi huyo aliyefariki dunia Machi 17, 2021, ikiwa ni zaidi ya miezi mitatu baada ya kushika awamu ya pili ya uongozi wake.

Misa hiyo iliyofanyika katika viwanja vya JS Chato imeongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge – Ngara, Severine Niwemugizi, ilihudhuriwa na viongozi wa dini, viongozi wa Serikali, wastaafu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na mamia ya wananchi.

Wananchi mbalimbali wakati wa adhimisho la misa Takatifu ya kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania Hayati, Dk John Pombe Magufuli, inayofanyika leo Machi 17, 2026 Chato mkoani Geita.

 Akizungumza katika hadhara hiyo, Dk Nchimbi amesema kupitia uongozi wake, Magufuli aliweza kulea na kuinua viongozi wapya wengi, hususan vijana, waliopata nafasi ya kujifunza na kukua ndani ya mfumo wa uongozi wa nchi.

Amesema ikiwa Watanzania watayashika na kuyaendeleza mambo makubwa aliyoyafanya Magufuli, wataweza kumuenzi kwa vitendo na kuendeleza maono yake ya kujenga taifa linalojitegemea.

“Kutoka kwa hayati Magufuli tunajifunza wito wa kila Mtanzania kujitoa na kufanya kazi kwa bidii. Alijitambulisha kwa falsafa yake ya Hapa Kazi Tu, akiamini kila mmoja anapaswa kujituma na kutoa mchango wake kwa taifa kupitia kazi,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, Magufuli aliamini kuwa kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kiwango cha juu ndiyo njia pekee itakayoiwezesha Tanzania kujinasua kutoka katika umaskini.

Ameongeza kuwa katika uongozi, Watanzania wanapaswa kujifunza ujasiri na uthubutu aliokuwa nao Magufuli katika kufanya maamuzi magumu yaliyolenga masilahi ya taifa.

“Alitufundisha umuhimu wa kuwajibika na kusimamia misingi ya haki na usawa katika kuwahudumia wananchi wote. Hakuyumbishwa katika kupiga vita uzembe wala rushwa,” amesema.

Aidha, Dk Nchimbi amesema Magufuli alikuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa kujitegemea kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, akieleza kuwa hatima ya maendeleo ya bara hili ipo mikononi mwa wananchi wake wenyewe.

Viongozi wengine wamzungumzia

Akizungumza kwenye kumbukumbu hiyo Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango amesimulia kwa sauti ya utulivu lakini yenye hisia, akimkumbuka kiongozi huyo aliyemfundisha kumtegemea Mungu na kusimamia fedha za umma kwa nidhamu isiyoyumba.

Amesimulia kuwa wakati fulani alipokuwa akisumbuliwa na maumivu ya mgongo, alimweleza Magufuli kuhusu hali hiyo.

Badala ya kumpa ushauri wa kawaida tu, Rais huyo wa zamani alimpatia zawadi ya kitabu cha maombi ya rozari (mawaridi) na hata kuwatafuta masista kutoka Karagwe ili wamuombee.

Simulizi hilo halikuishia hapo, amesema wakati alipokuwa akiugua, Magufuli aliendelea kuonyesha upendo wa karibu wa kifamilia, hata kumshirikisha mkewe, Janeth Magufuli, katika kumuombea.

Pia, Mpango anakumbuka Magufuli kwa niidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwamba ilikuwa muhimu zaidi, akisimulia kisa kimoja cha kukata masurufu ya viongozi.

 “Kulikuwa na orodha ndefu ya viongozi waliokuwa wamepangwa kusafiri nje ya nchi. Kwa kuwa gharama zilionekana kuwa kubwa, niliona ni busara kwanza kupata mwongozo wa Rais, alipoiangalia orodha hiyo, aliikata kuanzia tarehe za safari hadi idadi ya watu waliokuwa wanafuatana na viongozi hao,” amesema.

Majaliwa akumbuka uzalendo

Waziri Mkuu mstaafu Kassim Majaliwa amesema Magufuli alikuwa kiongozi aliyethamini uwajibikaji, uadilifu na matokeo ya kazi, sifa ambazo zilijenga taswira yake kama mtumishi wa wananchi.

“Leo hii tupo hapa kwenye kumbukizi hii, hatuwezi kujitenga na sifa hizi kwa Dk Magufuli… alikuwa ni kiongozi mzalendo na uzalendo wake ulijengwa juu ya misingi ya uwajibikaji, uaminifu na dhamira ya kuona taifa linapiga hatua za maendeleo,” amesema.

Majaliwa ameeleza kuwa hayati Magufuli alikuwa mtu mkweli na mwenye msimamo mkali katika kusimamia maadili ya uongozi, akiwakemea vikali wale waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu.

“Hayati alikuwa ni mtu mkweli, lakini pia alikuwa hana mzaha katika mambo yake na ni mkali. Alikemea maovu, wezi, wala rushwa na wabadhirifu wa mali za umma. Yeyote ambaye hakufuata misingi hii aliachana naye, huo ndio ulikuwa utaratibu wake,” amesema.

Majaliwa amesema mbali na kuwa Rais, Magufuli alikuwa pia mwalimu kwa viongozi waliokuwa wakifanya kazi naye, jambo lililowawezesha kupata uzoefu na mafunzo ya uongozi.

Amesema mafunzo hayo yameendelea kuonekana hata baada ya kifo chake, ambapo miradi mingi ya kimkakati aliyoianzisha, imeendelea kutekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Magufuli alikuwa pia mwalimu. Tuliyekuwa naye jirani kwa kipindi kirefu tulijifunza mengi kutoka kwake katika kipindi chake. Na hii ndiyo iliyopelekea hata alipotangulia mbele ya haki na Rais Samia kuingia madarakani, aliweza kutekeleza miradi yote ya kimkakati iliyoachwa na marehemu,” amesema.

Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dk Doto Biteko, amesema hayati Magufuli alikuwa kiongozi aliyejituma sana kwa kufanya kazi usiku na mchana.

Ameeleza kuwa kupitia utendaji huo, aliwaachia viongozi wa Awamu ya Sita mahali pazuri pa kuanzia, huku akiwataka Watanzania kuendelea kumuenzi kwa vitendo.

Akiwasilisha salamu kwa niaba ya Bunge, Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo amemtaja kiongozi huyo kama mwasisi wa miradi mikubwa iliyokuwa ikionekana kuwa migumu kutekelezeka, ikiwemo reli ya kisasa, Bwawa la Mwalimu Nyerere, miundombinu ya barabara na daraja la Busisi.

Akizungumza kwa niaba ya CCM, Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa (Bara), Stephen Wasira amesema hayati Magufuli alikuwa na uthubutu mkubwa katika kufanya maamuzi ambayo wengine wasingeweza kuyatekeleza, akitolea mfano wa uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma.

Aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wakati wa Magufuli, Jenerali Venance Mabeyo, amewahimiza Watanzania kuendeleza ndoto za hayati Magufuli kwa kuendeleza yale aliyoyaanzisha na aliyoyakusudia, ili kufikia Tanzania bora yenye mafanikio ya sasa na baadaye.

Akizungumza kwenye misa hiyo Askofu wa Jimbo Katoliki Geita, Flavian Kasala amesema kuendelea kukutana katika misa takatifu kwa ajili ya kumkumbuka kiongozi huyo kunaonyesha wazi jinsi familia na waumini wanavyoamini na kuthamini umoja na wale waliotangulia mbele ya haki.

Askofu Kasala ambaye amezungumza kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), amesema kumbukumbu hiyo ya kiimani imekuwa ishara ya matumaini kwa wengi, ikionyesha namna ambavyo waumini wanaendelea kuungana kiroho na wapendwa wao waliowatangulia.

“Familia kuendelea kumbuka kwa misa takatifu imeonyesha wazi jinsi ambavyo inaamini na kupenda kuendelea kuungana na wapendwa wetu waliotutangulia ili adhimisho hili liwe sehemu kubwa ya tumaini lao,” amesema Askofu Kasala.

Ameongeza TEC inaendelea kuwatia moyo waumini na Watanzania kwa ujumla kuendeleza utamaduni wa kumuombea marehemu huyo kwa njia ya misa takatifu na sala huku ikitambua mchango alioutoa katika maendeleo ya taifa.

Askofu Kasala amesema matendo aliyoyafanya Magufuli kwa taifa bado yanaonekana hadi leo, jambo linalowafanya Watanzania wengi kuendelea kumuenzi na kuyathamini matunda ya uongozi wake.