Dar es Salaam. Mkataba wa makubaliano uliosainiwa kati ya Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Benki ya TIB umetajwa kuwa hatua muhimu itakayoiwezesha Tanzania kuimarisha vyanzo vya ndani vya maendeleo na kupunguza utegemezi wa wafadhili wa kimataifa.
Makubaliano hayo ya miaka minne yanalenga kuendeleza mifumo bunifu ya ufadhili wa maendeleo, itakayochangia mageuzi ya kijamii na kiuchumi nchini kwa kufungua fursa mpya za kuibua na kuendeleza miradi yenye tija na inayoweza kuvutia uwekezaji, sambamba na vipaumbele vya taifa.
Maeneo ya kipaumbele yatakayolengwa ni pamoja na nishati jadidifu, maendeleo ya biashara ndogo na za kati, uchumi wa buluu, pamoja na miradi inayoongozwa na vijana.
Lengo ni kuongeza utayari wa uwekezaji, kuhamasisha mifumo ya ufadhili mseto na kuchochea ukuaji wa uchumi jumuishi.
Akizungumza baada ya kusaini makubaliano hayo leo, Machi 17, 2026, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Shigeki Komatsuba, amesema hatua hiyo inakuja wakati ambapo mazingira ya ufadhili wa maendeleo duniani yanabadilika kwa kasi, huku misaada ya ruzuku ikizidi kupungua.
“Lengo ni kuunganisha nguvu na utaalamu ili kuharakisha utekelezaji wa miradi yenye tija na yenye uwezo wa kuvutia uwekezaji na kusaidia kupunguza hatari za uwekezaji, kuvutia mitaji kutoka sekta binafsi na wawekezaji wa kimataifa, pamoja na kujenga mfumo imara wa kifedha unaoweza kuhimili mabadiliko ya kiuchumi,” amesema.
Amesema ushirikiano huo unatoa fursa kwa Tanzania kujenga uchumi unaojitegemea zaidi, unaotegemea rasilimali za ndani na ubunifu, huku ukilenga kuhakikisha kuwa uwekezaji unaleta matokeo chanya kwa wananchi kupitia ajira, biashara imara na maendeleo endelevu.
Komatsuba amesema mabadiliko hayo ni chanya, kwani yanafungua fursa nyingi ndani ya nchi, wakati ambapo uchumi wa kipato cha kati unapaswa kuendeshwa na rasilimali za Watanzania, kwa Watanzania na kwa manufaa ya Watanzania.
“Hii inatulazimu kufikiria upya namna tunavyokusanya na kusimamia rasilimali, na pia kubadilisha namna taasisi za fedha na washirika wa maendeleo wanavyofanya kazi,” amesema.
Amesema ushirikiano huo unaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050), pamoja na juhudi za Serikali za kuharakisha mageuzi ya kiuchumi endelevu, kuimarisha fursa za uwekezaji na kulinda rasilimali za mazingira.
“Tunaleta uwezo wa ziada unaojumuisha utaalamu wa sera, uandaaji wa miradi, viwango vya mazingira, kijamii na utawala, pamoja na zana za kuoanisha miradi na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Pia tuko tayari kuunganisha TIB na wadau wengine kama sekta binafsi, vyuo vikuu na wawekezaji wa kimataifa,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo TIB, Deogratius Kwiyukwa, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimkakati katika kufungua fursa za ufadhili wa maendeleo endelevu.
“Ushirikiano huu kati ya Benki ya Maendeleo TIB na UNDP unaakisi maono ya pamoja ya kuharakisha maendeleo endelevu nchini Tanzania.
“Kama taasisi ya kifedha yenye dhamana ya kutoa mikopo katika miradi ya maendeleo, TIB inaendelea na utoaji wa mitaji ya muda mrefu pamoja na suluhisho bunifu za kifedha zitakazochochea uwekezaji wenye mageuzi katika sekta muhimu za uchumi wetu,” amesema Kwiyukwa.
Amesema ushirikiano huo pia unaonesha kuimarika kwa imani ya washirika wa maendeleo wa kimataifa kwa uwezo wa Benki ya Maendeleo TIB katika kubuni, kuandaa na kutekeleza ufadhili wa miradi ya maendeleo yenye athari chanya kwa uchumi.
