Shinyanga. Zaidi ya watoto 781,186 wenye umri wa miaka sifuri hadi 10, wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya polio mkoani Shinyanga ili kuwazuia kupata virusi vya ugonjwa huo.
Hayo yamebainishwa leo Machi 17, 2026 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndungile wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kutoa chanjo ya polio kuanzia Machi 24 hadi 27, 2026 kupitia vituo vya afya, nyumba kwa nyumba, vituo vya kulelea watoto mchana (daycare) pamoja na shuleni.
“Utafiti uliofanyika jijini Mwanza umeonyesha kuwa maji taka yana vimelea vya virusi vya polio na ndiyo maana Serikali imeona umuhimu wa kuwapatia chanjo watoto hao ili kuwanusuru na ulemavu wa kudumu na vifo, ambapo walengwa katika mkoa huu ni watoto takribani 781,186,” amesema Dk Ndungile.
Dk Ndungile amesema kampeni hiyo itafanyika kwenye mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ipo kwenye hatari ya kusambaa kwa vimelea na kuwaweka hatarini watoto, hivyo Serikali imeona ni vema kuanza kuzuia kwa kuwapatia chanjo mapema kabla madhara hayajawa makubwa.
Mratibu Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Shinyanga, Moses Mwita amesema ugonjwa wa polio umekuwa tishio kwa miaka mingi ambapo Tanzania kwa mara ya mwisho mtu aliyegundulika na ugonjwa huo ni mwaka 1996, hivyo Serikali imekuwa ikitoa chanjo hiyo kwa watoto wa umri tofauti.
Mwita amesema chanjo ya polio inatolewa bure na itatolewa kwa njia ya matone na siyo sindano ambapo wataalamu watapita kwenye kila nyumba kuanza kuhamasisha, lengo ni watoto wote waliokusudiwa wapate chanjo hiyo kwani haina madhara yoyote.
“Hii chanjo inatolewa kwa mikoa saba ambayo ni Mwanza, Singida, Mara, Tabora, Simiyu, Geita na Shinyanga ambapo baada ya uzinduzi huu wa ngazi ya mkoa, kila halmashauri itafanya shughuli hiyo na kuwafikia watoto waliolengwa, tayari wataalamu wamepatiwa maelekezo,” amesema Mwita.
Mtoa elimu kwa umma idara ya kinga kutoka Wizara ya Afya, Anne Shuma amesema waandishi wa habari wanategemewa kuhamasisha na kufikisha ujumbe kwa wananchi ambapo hakuna mgonjwa wa polio wala mlipuko wa polio.
Hata hivyo, amesema kuna vimelea na Serikali imeanza kuchukua tahadhari kuwawekea kinga hata kama alikwisha chanjwa atarudia tena.
