Huduma za afya CCBRT zatikiswa, sababu zatajwa

Dar es Salaam. Dalili za kuyumba kwa baadhi ya huduma zimeanza kuonekana katika Hospitali ya CCBRT, inayojulikana kwa huduma za matibabu maalumu ya wenye ulemavu na uzazi kutokana na changamoto za kifedha.

Ugumu unaopitiwa na hospitali hiyo iliyopo Msasani jijini Dar es Salaam, ni katika utoaji wa huduma bure kwa watu wenye matatizo ya macho, mguu kifundo, tiba mazoezi na mifupa huduma ambazo zilikuwa zinagharimiwa na wafadhili.

Mpaka sasa ni huduma maalumu ya matibabu ya fistula ya uzazi ambayo imeendelea kutolewa bila malipo, licha ya kupungua kwa ufadhili, ikijumuisha upasuaji, usafiri, chakula na malazi kwa wahitaji.

Hali hiyo inakuja ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza nchi yake kusitisha misaada ya maendeleo kwa nchi mbalimbali, jambo ambalo liliathiri mashirika mengi yanayotegemea misaada kutoka Marekani, hususan kwa miradi ya kilimo na afya.

Alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi amesema suala la kupungua kwa ufadhili wa wadau, si changamoto ya hospitali hiyo pekee, lakini huduma nyingine zinaendelea kutolewa.

“Kama ni mwandishi mzuri utafahamu tu kwamba ni taasisi nyingi tu zimefungwa kwa sababu ya changamoto ya ufadhili,” anasema Msangi na kuongeza:

“Ile athari (kukosa ufadhili) imeathiri taasisi nyingi na CCBRT ni moja wapo, sisi ni taasisi ambayo tulikuwa tunapata ufadhili wa wageni kuanzia mwaka 1994, kwa hiyo tunaendelea kutoa huduma.”

Alipoulizwa madai ya kusitisha huduma kwa Jumamosi na Jumapili, Msingi alisema zinatolewa kama kawaida lakini kwa siku ya Jumapili huduma huishia saa nane mchana.

“Kama ni kuondolewa huduma za bure, hii ni kutokana na kupungua kwa baadhi ya wahisani wetu. Kwa wale waliokuwa hawachangii kabisa, tumepata hiyo changamoto kwa sababu ufadhili tuliokuwa tunapata umeathirika,” anafafanua Msangi.

Machi 5 mwaka huu, kuanzia saa 1 asubuhi hadi saa 8 mchana gazeti hili lilishuhudia idadi ndogo ya wagonjwa waliofika na kutibiwa, tofauti na miezi kadhaa nyuma.

Uchunguzi wa Mwananchi kwa siku tofauti ulithibitisha idadi ndogo ya wagonjwa katika vitengo mbalimbali, ikiwemo mazoezi tiba, ambako baadhi ya wagonjwa waliokutwa walisema wamepunguza siku za kwenda hospitalini kutokana na kukosa fedha za malipo.

Enesta Daudi (22) ni miongoni mwa kinamama wenye watoto wenye changamoto, ambao hufika hospitalini hapo kwa ajili ya mazoezi tiba ya mtoto wake Daylan (3).

Anasema kwa sasa kuna ongezeko la gharama za matibabu ikilinganishwa na zamani, suala linalowafanya walio wengi kufika kituoni mara moja kwa wiki kutokana na kukosa fedha.

“Zamani tiba mazoezi ilikuwa bure, ikaanza kuwa Sh2, 000 na sasa imefika Sh20, 000. Kuna kipindi mwaka jana gharama ilipanda mpaka kufikia Sh50,000 wengi walishindwa kulipia, alijitokeza mfadhili akalipia Sh30,000 kwa hiyo sisi tunaendelea kuchangia Sh20,000 ile ile,” anasema.

Enesta mkazi wa Kibaha mkoani Pwani, anaeleza: “Mwanangu angekuwa amekaa sawa. Lakini nilisimama matibabu baada ya gharama kuongezeka, nikaanza tena mwaka jana mwishoni, nakuja kwa wiki mara moja ila kama ningeweza ningekuja kila siku.”

Baadhi ya kinamama waliofika walisema wanalazimika kuendelea na kliniki kutokana na huduma nzuri, wengine wakisema wanafuata wataalamu, licha ya kwamba huduma hiyo bado kwao ni ghali.

Ongezeko la gharama pia limetajwa katika kitengo cha huduma za mguu kifundo na mwandishi alipouliza kuhusu hali hiyo, mhudumu aliyekutwa alijibu:

“Kwa sasa huduma zote zinatolewa kwa malipo kuanzia kumuona daktari na huduma nyinginezo. Ukija na mtoto mwenye hiyo changamoto uandae gharama zote za matibabu,” alijibu mhudumu huyo kwa kifupi.

Pamoja na huduma hizo, baadhi ya watumishi wameiambia Mwananchi kuwa suala la mishahara nalo limekuwa changamoto kwa wakati huku baadhi ya watumishi wakielezwa kuondoka.

Hata hivyo, CEO Msangi alipoulizwa alisema hakuna kitu kama hicho.

“Mshahara wa Desemba mwaka jana tulilipwa Januari 15, kuna wafanyakazi wenzetu baadhi wameondoka kutokana na hali kuwa mbaya,” amesema mmoja wao.

Mfanyakazi mwingine ambaye pia hakutaka kuandikwa jina lake, amesema hali ya kifedha hospitali hapo imebadilika kutokana na wafadhili kubadili vipaumbele.

Anasema kwenye huduma za macho na mifupa ambazo wafadhili hao walikuwa wakiwezesha nako wameacha na kusababisha upungufu kwa baadhi ya wataalamu waliokuwa wakitoa huduma hizo.

Amesema vipaumbele vya wafadhili vimebadilika na pia taasisi zinazotegemea wafadhili zimekuwa nyingi, hivyo kuna hali ya ushindani wa kugombania wadau hao.

“Jumamosi na Jumapili huduma zilikuwa zikitolewa hadi saa nane, wagonjwa wa dharura walikuwa wakihudumiwa, sasa kwa siku hizo hakuna huduma. Kwa wale wagonjwa wa nje wanaolipia huduma bado wanapokelewa,” anasema.

Huduma za macho zaathirika

Kutokana na kuondoka kwa wafadhili, hata kitengo hicho cha macho kilichokuwa kimbilio gharama zake zimeendelea kuongezeka kuanzia kuona daktari, upasuaji na huduma za miwani.

Geofrey Lyimo (48), mmoja wa wagonjwa waliofika hospitali hapo kubadili miwani, amezungumzia ongezeko la gharama.

“Nimekuwa nikibadili miwani mara moja kila mwaka na bajeti yangu nikiwa na Sh200,000 nitamuona daktari, nitapata vipimo, fremu na lenzi. Lakini, safari hii miwani peke yake yaani fremu na lenzi imenigharimu Sh400,000 na hapo bado fedha nilizomuona daktari na vipimo,” anasema Lyimo.

Naye Pili Athuman (35) amesema kutokana na ongezeko la gharama za miwani, aliishia kumuona daktari na vipimo huku akipanga kwenda kuchukua miwani katika hospitali nyingine.

“Kwa gharama ya miwani yangu ni zaidi ya Sh500,000 kwa hiyo nimeona afadhali nichukue vipimo hapa niende Hospitali ya Mnazi Mmoja huenda nitapata nafuu ya gharama,” anasema Pili.

Jumanne anasema kuwa miwani yake yenye lenzi 0.75 aliyonunua mwaka 2018 kwa Sh330,000 ikijumuisha upimaji wa macho, mwaka huu aliporudi alipaswa kulipa Sh450,000.

“Hili ni ongezeko la gharama ambalo limezidi uwezo wangu wa kifedha, gharama hizi ni kwa ajili ya vipimo na miwani, hivyo ninasubiri watoto wangu wanipatie fedha ili niweze kupata huduma hii,” amesema.

Juma Madodi, anasimulia ilivyochukua zaidi ya mwezi kupata huduma ya miwani kwa ajili ya changamoto ya uoni, ambayo hata hivyo imeshindikana, huku akihusisha na hali hiyo.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya, Amour Amour kufahamu ni namna gani Serikali itaisaidia Hospitali ya CCBRT kutokana na wahisani kuondoka, alisema hospitali ya hiyo si mali ya Serikali, hivyo wanachofanya ni kuingia makubaliano nao ya namna ya kufanya kazi.

“Ili tuweze kufanya kazi pamoja lazima tuingie makubaliano, kwa hiyo tupo kwenye majadiliano ya makubaliano,  tukifika mwisho tutaendelea nao,” anasema.