Mwanza. Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela washtakiwa watano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya ugaidi, huku bunduki tatu aina ya AK-47 zikikabidhiwa kwa Jeshi la Polisi.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Godfrey Isaya wa Mahakama hiyo, Masjala Ndogo ya Mwanza, kulibainika pia kuwapo kwa mkanganyiko ambapo katika ukurasa wa 43 wa hukumu, mshtakiwa wa tatu, Mswadiki Mtaburu, alitajwa kutiwa hatiani, lakini wakati wa kutamka adhabu katika ukurasa wa 47, jina lake halikutajwa miongoni mwa waliohukumiwa.
Waliohukumiwa katika shauri hilo namba mbili la mwaka 2022 ni Mnawala Hamisi, Mustafa Hamisi, Hamisi Kitigani, Abdalah Rashid na Zulfa Abdutwalibu. Awali walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, lakini kutokana na kukaa mahabusu kwa muda mrefu tangu mwaka 2016, adhabu yao ilipunguzwa na sasa wanapaswa kutumikia kifungo cha miaka 10.
Mbali na adhabu hiyo, mshtakiwa wa pili, Mustafa Hamisi, pamoja na mshtakiwa wa tisa, Zulfa Abdutwalibu, walipatikana pia na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria, na hivyo kuongezewa kifungo cha miaka mitano jela. Hata hivyo, adhabu hizo zitaanza kutumika kwa pamoja (concurrent sentences).
Katika hukumu hiyo iliyotolewa Machi 13, 2026 na kuwekwa wazi Machi 16, 2026, washtakiwa wanne ambao ni Mwantumu Ramadhan, Mussa Shabani, Asia Juma na Mayasa Twaha waliachiwa huru baada ya Mahakama kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha tuhuma dhidi yao.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 5, 2012 na Desemba 5, 2016 katika Wilaya ya Nyamagana, Jiji la Mwanza na maeneo mengine nchini, washtakiwa hao walikula njama ya kuangusha Serikali ya Tanzania na kuanzisha dola la Kiislamu. Hata hivyo, waliposomewa mashitaka yao walikanusha tuhuma zote.
Ili kuthibitisha kesi yake, upande wa Jamhuri uliita mashahidi 13, ambao kwa sababu za kiusalama majina yao yalifichwa, na uliwasilisha vielelezo 29 mahakamani. Vielelezo hivyo vilijumuisha bunduki tatu za AK-47, magazini nane za bunduki hizo, risasi 51, maganda ya risasi sita, pamoja na magazini tano zenye risasi 30 kila moja. Pia kulikuwa na vifaa vingine kama majambia, visu na maelezo ya onyo kutoka kwa baadhi ya washtakiwa.
Ushahidi uliotolewa ulieleza kuwa katika kipindi hicho, Jiji la Mwanza lilishuhudia ongezeko la matukio ya uhalifu usio wa kawaida, ikiwa ni pamoja na uporaji wa kutumia silaha na mauaji ya viongozi wa mitaa. Moja ya matukio hayo ni mauaji ya mwenyekiti wa mtaa wa Buhongwa, yaliyosababisha kufunguliwa kesi ya mauaji namba 224 ya mwaka 2021, ambayo baadaye iliondolewa kabla ya upelelezi kubaini uhusiano wake na ugaidi.
Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa nane aliyefichwa kwa utambulisho wa herufi āPā, mwanzoni mwa mwaka 2016 alipokea taarifa za kuwepo kwa kundi la watu waliokuwa wakikusanya fedha katika misikiti mbalimbali jijini Mwanza kwa madai ya kuwasaidia wenzao waliokuwa gereza la Butimba wakikabiliwa na kesi za ugaidi. Ilidaiwa kuwa fedha hizo zilikuwa zikikusanywa kwa lengo la kusaidia shughuli za kigaidi, zikiwamo za kundi la Islamic State (IS).
Baada ya taarifa hizo, Jeshi la Polisi lilianzisha operesheni ya upelelezi iliyohusisha maofisa wa intelijensia na watoa taarifa. Mnamo Novemba 24, 2016, mmoja wa washtakiwa alikamatwa katika kituo cha mabasi cha Rwegasore, na katika mahojiano alitaja washirika wake, jambo lililosababisha kukamatwa kwa wengine.
Katika operesheni hiyo, Polisi walikamata silaha mbalimbali, huku kukiwa na makabiliano ya risasi na tukio la kurushwa kwa bomu la mkono. Pia wataalamu wa mabomu walifanikiwa kutegua bomu aina ya F-1 Russian lililokuwa limehifadhiwa katika moja ya nyumba za washukiwa. Upelelezi uliwafikisha hadi Uvinza mkoani Kigoma ambako walipata bunduki zaidi, risasi, na vifaa vya kijeshi kama darubini (binoculars).
Katika utetezi wao, washtakiwa walikana kuhusika na makosa hayo na kudai walikamatwa bila sababu za msingi. Baadhi yao walidai kulazimishwa kusaini nyaraka bila kupewa nafasi ya kuzisoma, huku wengine wakidai kupigwa na Polisi wakati wa mahojiano. Pia walieleza kuwa awali walikuwa wakikabiliwa na kesi za mauaji kabla ya kubadilishiwa mashtaka na kuwa ya ugaidi.
Akitoa hukumu, Jaji Isaya alisema baada ya kuchambua ushahidi wote, Mahakama imejiridhisha kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kuthibitisha baadhi ya makosa dhidi ya washtakiwa waliotiwa hatiani, hususan kosa la kula njama ya kutenda ugaidi. Hata hivyo, alibainisha kuwa kwa baadhi ya washtakiwa na baadhi ya makosa, ushahidi haukutosha na hivyo wakaachiwa huru.
Pia Mahakama iliamuru kuwa silaha zote, risasi na vifaa vingine vilivyokamatwa na kuwasilishwa kama vielelezo vibaki chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi.
