Kutupa laini hakufuti deni, wananchi waonywa athari za kifedha

Dodoma. Wimbi la baadhi ya wananchi kukopa fedha kupitia laini za simu zilizosajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa (Nida) kisha kuzitupa ili kukwepa madeni, limeibua tahadhari kuhusu athari za muda mrefu kwenye rekodi za kifedha.

Ingawa hatua hiyo huonekana kama njia ya mkato, wataalamu wa fedha wanaonya kuwa deni hubaki hai na huendelea kumwandama mkopaji anapojaribu kupata huduma za kifedha. Uchunguzi unaonyesha baadhi ya watu hukopa kupitia simu na wanaposhindwa kulipa, hutupa laini na kusajili nyingine mpya wakiamini wamejinasua, lakini taarifa za mikopo huhifadhiwa kwa kutumia Nida hivyo deni halifutiki.

Mkazi wa Dodoma, Merina Jackson (si jina halisi), amesema alikopa kupitia simu lakini alichelewesha kulipa deni la Sh74,000 kutokana na changamoto za kifedha. Baadaye alipohitaji mkopo benki kwa ajili ya ada na kodi ya nyumba, alikataliwa kwa sababu ya deni hilo. “Nililazimika kulipa kwanza ndipo nikapata mkopo,” amesema.

Kwa upande wake, dereva wa bodaboda, Jeremia Makomelo, amekiri kutupa laini kila alipokuwa na deni kubwa akidhani anajinasua. Hata hivyo, alishindwa kupata mkopo wa kikundi na hata kufungua akaunti benki kutokana na rekodi mbaya. Anasema alikuwa anadaiwa hadi Sh600,000 kwenye laini tatu tofauti kabla ya kuanza kulipa kidogo kidogo kurekebisha hali yake.

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Kennedy Komba amesema kutupa laini hakufuti deni bali huongeza tatizo. Ameeleza kuwa taasisi za fedha huwasilisha taarifa za wakopaji kwenye ofisi za marejeo ya mikopo (CRB) kwa kutumia taarifa za Nida, jambo linaloweza kumzuia mkopaji kupata mikopo benki, taasisi ndogo, Saccos au huduma za simu.

Ameongeza kuwa riba na adhabu huendelea kuongezeka kadri deni linavyocheleweshwa. Kisheria, kutolipa mkopo si kosa la jinai bali ni madai ya kiraia, ambapo taasisi zinaweza kufungua kesi au kuwasilisha taarifa CRB.

Ameshauri wananchi kuwa wazi kwa wakopeshaji wao wanapopata changamoto na kuepuka kukopa mkopo mwingine kulipia wa awali, kwani huongeza mzigo wa madeni.