Viongozi ACT Wazalendo wadaiwa kukamatwa na Polisi Kagera

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Janeth Rithe inadaiwa  amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera alikokwenda kwa ziara ya kikazi ya chama hicho. 

Rithe inadaiwa amekamatwa pamoja na Naibu Katibu wa Ngome ya Wanawake ya chama hicho, Severina Mwijage, waliokuwa pamoja katika ziara hiyo.

Taarifa ya kukamatwa kwa Rithe na Severina, imetolewa leo Jumanne Machi 17, 2026 na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo.

Akizungumza na Mwananchi, Shangwe amedai wawili hao wamekamatwa wakiwa katika Kijiji cha Bwera, Kata ya Buyango mkoani Kagera na askari waliojitambulisha kuwa wametumwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Missenyi. 

“Tumepokea taarifa za kukamatwa kwa viongozi wetu, hawa wamekamatwa baada ya ibada ya kumuombea marehemu Dafroza Jakob, nyumbani kwao Kagera,” amedai.

Dafroza alikuwa diwani wa Sirari kwa tiketi ya ACT Wazalendo na alifariki dunia Novemba 5, 2025 alipokuwa akichukuliwa maelezo katika Kituo cha Polisi.

Taarifa ya Jeshi la Polisi ilieleza kifo chake kilitokana na kuugua ghafla wakati alipokuwa akichukuliwa maelezo, hali iliyosababisha apelekwe hospitali na baadaye akafariki akiwa anapatiwa matibabu.