DAR City ikiwa katika maandalizi kwa ajili ya Ligi ya Kikapu Africa (BAL) 2026, meneja wa timu hiyo, Simon Joe amesema wanajipanga kufanya makubwa katika mashindano hayo wakilenga kutoa ushindani wa hali ya juu na kuandika rekodi mbalimbali.
Mashindano ya BAL yamepangwa kuanza Machi 27, mwaka huu, yakiwa yamegawanywa katika makundi mawili yatakayochezwa katika nchi tofauti.
Joe ameliambia Mwanaspoti kuwa timu hiyo kwa sasa imejichimbia mjini Zanzibar na wachezaji wake wameahidi kufanya vizuri wakilenga kuandika historia mpya kwa timu za Tanzania itakayofanya vizuri na kufika mbali.
“Kupitia mashindano haya naamini Dar City itatumia nafasi hiyo pia kuitangaza Tanzania kupitia mchezo wa kikapu,” alisema Joe.
Taarifa iliyotolewa na wasimamizi wa mashindano ya BAL ilieleza kundi la Kalahari Conference lililopangwa Afrika Kusini litakuwa na timu za Dar City (Tanzania), Petro de Luanda (Angola) na Al Ahly Benghazi (Libya), APR (Rwanda), Nairobi City Thunder (Kenya) na Johannesburg Giants (Afrika Kusini).
Nalo kundi la Sahara Conference litakuwa na Fath Union Sport (Morocco), Al Ahly (Misri), ASC Ville de Dakar (Senegal), Club Africain (Tunisia), JCA Kings (Côte d’Ivoire) na Maktown Flyers (Nigeria), litafanyika nchini Morocco.
Timu ya mpira wa kikapu ya Dar City ilipewa nafasi (Wild Card) ya kucheza mashindano ya Basketball Africa League (BAL), baada ya kuonyesha kiwango kikubwa katika mashindano ya Road to BAL Elite 16 nchini Kenya.
Baada ya timu hiyo kuonyesha kiwango kizuri, maofisa wa BAL waliipa nafasi timu ya Dar City kutokana na ubora wa uchezaji wake ulioonyeshwa katika mashindano hayo.
Dar City ilianza kampeni yake hiyo baada ya kufuzu kundi D la mashindano ya Road to BAL Divisheni ya Mashariki katika uwanja wa Shule ya Kimataifa IST (Masaki).
Katika mashindano hayo iliishinda timu ya Djabar ya Comoro kwa pointi 102-50 na timu ya Namuwongo Blazers kutoka Uganda kwa pointi 83-70.
Katika mashindano ya Road to BAL Elite 16 yaliyofanyika Kenya, Dar City iliishinda Bravehearts ya Malawi kwa pointi 93-75, Mtero Magic (Zambia) pointi 85-78 na Ferroviario da Beira (Msumbiji) kwa pointi 87-78.