Arusha. Umoja wa Wanasheria wa Pan-Africa (Palu) umeanza hatua za kutetea haki za urithi za wanawake wa Kiafrika wanaoishi katika ndoa zisizo rasmi, zinazojulikana kama “njoo tuishi,” pamoja na watoto wao ili kuhakikisha wanapata haki sawa za urithi.
Hatua hiyo imeanza leo Machi 17, 2026 jijini Arusha baada ya Palu kuwasilisha hati ya kuomba mwongozo na maoni ya kisheria katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kuhusu wajibu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu kulinda haki za wanawake na wasichana kulingana na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Palu, maoni ya kisheria kutoka Mahakama ya Afrika yatakuwa na umuhimu katika kusawazisha sheria za kitaifa na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, kuunda sera mpya na kuunga mkono jitihada za kupigania haki sawa za urithi kwa wanawake na wasichana barani Afrika.
Taarifa ya Palu iliyothibitishwa na Mkurugenzi wake, Donald Deya, mamilioni ya wanawake na wasichana wa Kiafrika bado wanakabiliwa na ubaguzi wa kisheria na wa tamaduni unaowapunguza katika kupata haki zao za urithi.
“Wanawake walioko katika ndoa zisizo rasmi, wajane na watoto waliozaliwa nje ya ndoa wapo hatarini zaidi kupuuzwa kutoka kwenye mifumo ya urithi,” inaeleza taarifa hiyo.
Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu wanawake, biashara na sheria ya mwaka 2026 inaonesha nchi 18 wanachama wa AU hazihakikishi haki sawa za urithi kwa watoto wa kiume na wa kike, wakati nchi 19 hazilindi haki sawa za wanawake na wajane.
Utafiti huo unaonesha kuwa, na haki thabiti za ardhi na urithi kwa wanawake kunaweza kuongeza mapato yao hadi mara 3.8, kuboresha upatikanaji wa mikopo na kupunguza uhaba wa chakula kwa zaidi ya theluthi moja ya kaya.
IMF na UN Women wanakadiria kuzibwa kwa mapengo ya kijinsia katika ushiriki wa kiuchumi, ikiwamo urithi, kunaweza kuongeza hadi Dola 7 trilioni za Marekani kwenye uchumi wa dunia.
Deya ametumia nafasi hiyo kuitaka Serikali, taasisi za AU, mashirika ya kiraia na wadau wote kuungana katika kutekeleza haki sawa za urithi, kuondoa mila na desturi za kibaguzi na kulinda heshima na haki za kila mwanamke na msichana wa Kiafrika ili kufanikisha nchi kufikia malengo yake ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
