Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamiihiyo, Dk Regina Malima akizungumza akati kamati hiyo ilipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa ukumbi wa mihadhara unaoendelea kwa kutumia mapato ya ndani ya taasisi.
******
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kuhakikisha inatoa fedha kusaidia kukamilisha miradi inayotekelezwa katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW).
Agizo hilo limetolewa jijini Dar es Salaam wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa ukumbi wa mihadhara unaoendelea kwa kutumia mapato ya ndani ya taasisi.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Regina Malima, amesema ISW inastahili pongezi kwa jitihada zake za kutoa elimu pamoja na kushirikiana na jamii katika shughuli za maendeleo.
Amesisitiza kuwa mradi huo unapaswa kukamilika kwa wakati na kuboreshwa ili uwe rafiki kwa makundi yote, hususan watu wenye ulemavu, ili kuendana na sera ya usawa wa elimu.
Aidha, amesema baadhi ya miradi inachelewa kutokana na changamoto za kifedha, hivyo wizara inapaswa kuingilia kati ili kuhakikisha utekelezaji unakwenda kwa ufanisi.
Amebainisha kuwa ujenzi wa ukumbi huo umefikia zaidi ya asilimia 80, hatua inayotia matumaini ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Kamati hiyo pia imeitaka taasisi kuzingatia mahitaji ya makundi maalum katika miundombinu yake ili kuhakikisha usawa wa fursa kwa wanafunzi wote.
Amesema ufinyu wa bajeti unaathiri utekelezaji wa baadhi ya miradi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na makazi ya watumishi.
Ameongeza kuwa ukumbi huo utakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 na utasaidia kuongeza udahili, kupunguza msongamano na kuboresha mazingira ya elimu.




