UONGOZI wa Kaizer Chiefs ya Afrika ya Kusini, umeanza kumfuatilia mshambuliaji nyota wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga, Mzimbabwe, Prince Dube, ambaye mkataba wake na kikosi hicho unafikia tamati mwishoni mwa msimu huu.
Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa mabosi wa timu hiyo wanaangalia uwezekano wa kumpata mshambuliaji huyo, baada ya kupata ugumu wa kumsajili, aliyekuwa nyota wa Yanga, Mkongomani Fiston Mayele, anayecheza Pyramids FC ya Misri.
Lengo la kwanza kwa kikosi hicho, lilikuwa ni kumpata Mayele, ambaye anakumbukwa zaidi msimu wa 2022-2023, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga mabao 17, sawa na Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, aliyekuwa Simba.
Hata hivyo, licha ya Kaizer kuiwinda saini ya Dube, ila inaelezwa mabosi wa Yanga wako katika mazungumzo ya kumpa mkataba mpya wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho, huku mchakato huo ukiwa kwenye hatua nzuri kati ya pande hizo mbili.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Yanga, Julai 6, 2024, akitokea Azam FC, ambapo kwa msimu wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho 2024-2025, alifunga mabao 13, yaliyochangia pia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo. Msimu huu, nyota huyo ameifungia Yanga mabao sita ya Ligi Kuu.
Kwa mara ya kwanza, Dube alitua nchini Tanzania kucheza Ligi Kuu Bara akijiunga na Azam, Agosti 17, 2020, baada ya kuachana na Highlanders FC ya kwao Zimbabwe yenye makao yake mjini Bulawayo.
Katika misimu minne akiwa na Azam FC, Dube alifunga jumla ya mabao 33 ya Ligi Kuu, ambapo msimu wake wa kwanza wa 2020-2021, alifunga 14, msimu wa 2021-2022 akafunga moja, msimu wa 2022-2023 akatupia 11, kisha 2023-2024 akafunga saba.
