Serikali yatoa mwelekeo kwa kampuni zake zenye hisa chache

Arusha. Kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache zimetakiwa kujiendesha kwa ufanisi wa kibiashara, uwazi na mikakati madhubuti ili kuongeza mchango wake katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Wito huo umetolewa Machi 17, 2026 jijini Arusha na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar wakati akifungua mkutano wa wakurugenzi wa kampuni hizo (MIF 2026). Amesema Dira ya 2050 inalenga kukuza uchumi wa Tanzania kutoka dola za Marekani bilioni 85 hadi trilioni moja, jambo linalohitaji mchango mkubwa wa uwekezaji wa umma na binafsi.

Amesisitiza umuhimu wa mageuzi ya kiutendaji ili kuendana na mabadiliko ya uchumi wa dunia, ikiwemo matumizi ya teknolojia kuimarisha uwazi, ufanisi na imani ya umma. Pia ameitaka sekta ya umma na binafsi kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha malengo ya maendeleo.

Kwa mujibu wake, bodi za wakurugenzi na menejimenti zinapaswa kuoanisha mikakati ya kampuni zao na vipaumbele vya Taifa, huku zikizingatia ushindani wa masoko ya kimataifa. Aidha, viongozi wanapaswa kuwa na mtazamo wa kimkakati, unaoweza kutambua hatari na kutumia fursa mpya za kiuchumi.

Waziri Omar amesema Serikali inalenga kuongeza mapato yasiyotokana na kodi kutoka asilimia tatu hadi 10 ndani ya miaka mitano, sawa na takribani Sh5 trilioni kwa mwaka. Hili litategemea usimamizi bora wa uwekezaji na uongozi unaozingatia ubunifu na maamuzi ya haraka yanayotumia takwimu sahihi.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Uwekezaji, Fred Msemwa amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kupitia sera na sheria ili kuimarisha sekta binafsi.

Naye Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema jukwaa hilo limekuwa muhimu kwa viongozi kujadili utawala bora na utendaji wa kampuni hizo. Ameongeza kuwa uwekezaji wa Serikali umeongezeka kutoka Sh821 bilioni hadi Sh3.6 trilioni katika miaka mitano, huku gawio likipanda kutoka Sh58 bilioni hadi Sh266 bilioni.

Mkutano huo unawakutanisha zaidi ya wadau 200 kujadili namna ya kuboresha utendaji na mchango wa kampuni hizo katika uchumi wa Taifa.