Wabunge wa Somalia waapishwa kujiunga na Eala

Arusha. Hatimaye wabunge tisa kutoka Somalia wameapishwa rasmi kujiunga na Bunge la Afrika Mashariki (Eala), baada ya mvutano wa kisheria wa muda mrefu kuhusiana na mchakato wa uteuzi na changamoto za kifedha zinazoikabili Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Wabunge hao wameapishwa Machi 17, 2026 jijini Arusha ndani ya makao makuu ya Bunge hilo ambapo wanatarajiwa kuhudumu kwa muhula utakaohitimishwa Desemba 2027.

Kuapa kwa wabunge hao kunaashiria rasmi hatua muhimu ya kuimarisha ushiriki wa Somalia katika uongozi wa kikanda ndani ya EAC.

Wabunge wapya walioapa ni Abukar   Osman, Hussein  Abdi, Sahra  Hassan, Ilhan   Gasar, Fatima  Mahmoud, Abdisalam  Omar, Abdirahman  Sharif, Faisal   Roobke na Fahma   Noor.

Wabunge hao wamefikia hatua hiyo kufuatia mchakato wa uteuzi uliofanywa na Bunge la Shirikisho la Somalia mwishoni mwa mwaka 2025, kwa lengo la kuwawakilisha nchi yao katika mijadala ya kisheria na shughuli za kutunga sheria zinazounda ajenda ya kikanda ya EAC.

Mbele ya spika wa Bunge la Eala, Joseph Ntakiritumana, shughuli za uapisho zilifanyika katika kikao maalumu cha bunge hilo, ambapo washiriki walihudhuria kwa njia ya mtandao na ana kwa ana.

Somalia ilijiunga rasmi na EAC Novemba 2023 kama mwanachama wa nane, lakini haikuwahi kushiriki kikamilifu katika shughuli za Eala.

Kuapishwa kwa wabunge hao kunafuata baada ya uamuzi wa Januari 2026 wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) uliokataa agizo lililozuia mchakato wa uteuzi kutokana na migogoro ya uchaguzi.

Uamuzi huu uliwezesha wabunge hao wa Somalia kuanza rasmi kushiriki shughuli za Bunge leo rasmi.

Wabunge wapya sasa wanajiunga na wenzao kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), jambo ambalo linaimarisha uwakilishi wa kikanda katika Bunge hilo.

Mbali na wabunge hao, mawaziri watatu wapya wanaohusika na masuala ya EAC kutoka Tanzania, Rwanda na Somalia, pia, wameapishwa.

Mawaziri hao ni Mahmoud Thabit Kombo ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Ali Omar, Waziri wa Mambo ya Nje anayehusika na masuala ya EAC nchini Somalia na Yuta Kayetesi, Waziri wa Nchi anayehusika na masuala ya EAC nchini Rwanda.