Dar es Salaam. Shahidi wa 23 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Simon Mkondya, maarufu Dk Manguruwe na mwenzake Rweyemamu John, amedai alishawishika kuwekeza Sh10 milioni katika kampuni hiyo akiamini ni halali.
Shahidi huyo, Roselyn Kakolo, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Machi 17, 2026 kuwa alivutiwa kuwekeza baada ya kuona nembo ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), picha ya Rais na nyaraka za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizobandikwa ofisini, akiamini ni ishara ya uhalali.
Kakolo, mkazi wa Kigamboni na mfanyakazi mstaafu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), amesema aliwekeza fedha hizo kwa ajili ya kilimo cha soya katika ekari tano akiahidiwa faida ya Sh25 milioni ndani ya miezi sita. Ameeleza kuwa baada ya kulipa fedha kupitia akaunti ya Benki ya CRDB Desemba 20, 2022, alipewa risiti na kuambiwa kilimo kingeanza Januari 2023 mkoani Manyara.
Amedai kuwa alipofuatilia maendeleo ya uwekezaji wake, alipewa majibu ya jumla kuwa kilimo kinaendelea vizuri lakini hakuwahi kutumiwa picha au uthibitisho wowote. Baadaye mawasiliano yakawa magumu, huku Mkurugenzi wa kampuni akidai yuko safarini kabla ya simu zake kutopatikana kabisa.
Shahidi huyo ameeleza kuwa alipoenda ofisini alikutana na watu waliompa namba ya Mkondya, lakini juhudi zake za kumpata hazikufanikiwa. Baadaye ameelezwa kuwa ofisi ya Dar es Salaam imefungwa na kuhamia Dodoma, lakini alipojaribu kufuatilia huko hakukuta ofisi wala kupata mawasiliano yoyote.
Kutokana na hali hiyo, Kakolo aliripoti tukio hilo Jeshi la Polisi Tanzania kituo cha kati Dar es Salaam, ambako alielezwa kuwa watu wengi wamewasilisha malalamiko kama hayo. Aliandika maelezo na kuanza kufuatilia kurejeshewa fedha zake.
Mahakamani aliomba risiti ya malipo aliyofanya iwe sehemu ya ushahidi, na mahakama ilikubali kuipokea kama kielelezo.
Upande wa Jamhuri unadai uwekezaji huo uliendeshwa kwa mbinu zisizo halali zilizowasababishia hasara wawekezaji. Mkondya na mwenzake wanakabiliwa na mashtaka 126, ikiwemo kuendesha biashara ya upatu, huku Mkondya akikabiliwa pia na kosa la utakatishaji fedha.
Baada ya ushahidi huo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 26, 2026. Mkondya amerudishwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha lisilo na dhamana, huku mwenzake akiwa nje kwa dhamana.
