Shinyanga. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameagiza kutolewa kwa kibali cha kuruhusu ndege kutua wakati wa mchana katika Uwanja wa Ndege wa Mkoa wa Shinyanga ili kuharakisha kuanza kwa matumizi ya uwanja huo.
Akizungumza leo Machi 17, 2026 wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi wa uwanja huo uliopo katika Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga, Ulega amesema tayari majaribio ya kutua ndege yanaendelea, hivyo hakuna sababu ya kuchelewesha utoaji wa kibali hicho.
“Sasa hivi mko katika majaribio ya kutua ndege wakati wa mchana, basi kibali kitolewe ili kuruhusu ndege kutua na uwanja uanze kutumika mapema kwa lengo la kukuza uchumi wa nchi,” amesema Ulega.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads),
Mkoa wa Shinyanga, Ntuli Mwaikokesya amesema ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege umekamilika, huku kazi iliyobaki ikiwa ni ukamilishaji wa jengo la abiria.
Amefafanua kuwa jengo hilo liko katika hatua za mwisho na lina uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja. Aidha, alieleza kuwa njia ya kuruka na kutua ndege ina urefu wa kilomita 2.2 na upana wa mita 30.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi wa mkoa huo, hususan katika kurahisisha usafirishaji wa mazao ya biashara kama pamba.
Wakati huohuo, Waziri Ulega ameahidi kuwa Serikali itaanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kolandoto–Mhunze hadi Mangongo yenye urefu wa kilomita 53.6 katika Wilaya ya Kishapu, baada ya fedha kutengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.
Akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya barabara hiyo leo, Ulega amesema mradi huo utachochea shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kaskazini, hususan ile ya Shinyanga, Simiyu na Arusha pamoja na kuondoa changamoto za usafirishaji.
“Serikali inakusudia kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi vijijini na mijini. Mradi huu pia utaunganisha mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Arusha,” amesema Waziri Ulega.
Aidha, amewataka makandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji kwa kuongeza idadi ya wafanyakazi, saa za kazi na vifaa vya ujenzi, akisisitiza kuwa Serikali haitaongeza muda wa mradi huo.
Kwa upande wake, Mwaikokesya amesema barabara hiyo tayari imefanyiwa upembuzi yakinifu na maombi ya kibali yamewasilishwa wizarani ili kuruhusu kutangazwa kwa zabuni ya kumpata mkandarasi.
Amebainisha kuwa Sh413 milioni zimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa awali na baada ya kibali kutolewa, hatua inayofuata itakuwa ni kutangaza zabuni kwa makandarasi ili kuanza rasmi ujenzi.
Baadhi ya wananchi mkoani Shinyanga, akiwemo John Shija, ameomba barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli zao za kila siku.
“Barabara hii ikijengwa kwa kiwango cha lami itafungua fursa nyingi za kiuchumi, hususan katika usafirishaji wa mazao kama pamba, na pia kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo kufika Hospitali ya Kolandoto,” amesema Shija.
