MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE AITAKA MUHAS KUONGEZA KASI YA KUITANGAZA KAMPASI YA MLOGANZIL

*******

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko, amekitaka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kwa kushirikiana na Wizara, kuongeza kasi ya kuitangaza Kampasi ya Mloganzila kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea.

Mhe. Sekiboko ametoa rai hiyo Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwenye mradi wa ujenzi katika Kampasi ya Mloganzila.

Amesema kazi iliyofanyika ni kubwa, na kwamba nchi inakwenda kuzalisha wataalamu wabobezi katika maeneo mbalimbali ya tiba. Amesisitiza kuwa ni muhimu kampasi hiyo ifahamike kwa ubora wa elimu itakayotolewa pamoja na mchango wake katika kuboresha na kuongeza fursa za mafunzo na tafiti.

Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa majengo katika Kampasi ya Mloganzila unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 77, amesema mradi unaendelea vizuri ukiwa umefikia asilimia 80, na kwamba Kamati imeridhishwa na kasi pamoja na ubora wa kazi.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa, ikiwemo kuongeza udahili wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Pia amesisitiza kuwa upanuzi wa MUHAS utasaidia kupunguza uhaba wa madaktari na wataalamu wa afya nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Afya (MUHAS), Profesa Emmanuel Balandya, amesema eneo la Kampasi hiyo lina jumla ya ekari 3,800 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati pamoja na miradi mingine.

Profesa Balandya ameongeza kuwa kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaimarisha shughuli za ufundishaji, utafiti, pamoja na utoaji wa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo magonjwa ya moyo na mishipa ya damu pamoja na magonjwa ya mfumo wa fahamu.

Naye Msimamizi Msaidizi wa Mradi wa HEET katika Chuo cha MUHAS, Profesa Nathanael Siliri, amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa Kampasi ya Mloganzila ni kuifanya kuwa mji mkuu wa kitaaluma wa tiba, wenye vituo vya umahiri vitakavyotoa huduma za hali ya juu na kufanya tafiti zitakazochochea maendeleo ya sekta ya afya nchini na ukanda wa Afrika Mashariki.