Zoya: Binti wa miaka 14 anayepigania wasichana kubaki shuleni

Dar es Salaam. Methali isemayo “penye nia pana njia” inaakisi vyema safari ya Zoya-Fatimah Dewji (Zoya), msichana mwenye umri wa miaka 14 ambaye ameanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na hedhi – moja ya changamoto zinazowazuia wasichana wengi nchini Tanzania kuhudhuria masomo kikamilifu.

Licha ya kuwa bado ni mwanafunzi, Zoya ameanzisha kampeni iitwayo “Stay in School” inayojulikana kwa Kiswahili kama “Abaki Shuleni”, yenye lengo la kuwaelimisha wasichana kuhusu afya ya hedhi, kuwapatia vifurushi vya hedhi vinavyojumuisha pedi zinazoweza kutumika tena, pamoja na kuwajengea stadi muhimu za maisha ili kuwasaidia katika masomo na maisha yao kwa ujumla.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanaendelea na masomo bila kukatizwa. Taarifa kutoka kwa wadau wa sekta ya elimu zinaonyesha kuwa changamoto za hedhi shuleni ni kubwa zaidi kuliko watu wengi wanavyodhani.

Kwa wasichana wengi, suala hili limekuwa kikwazo kisichoonekana kinachowazuia kupata elimu ipasavyo.

Nchini kote, maelfu ya wasichana hukosa masomo kila mwezi kwa sababu hawana bidhaa salama za hedhi au wanahisi aibu na kukosa maandalizi wanapokuwa kwenye siku zao.

Kwa mujibu wa tafiti za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef) na washirika wa elimu nchini, baadhi ya wasichana hukosa kati ya siku tatu hadi tano za masomo kila mwezi wanapokuwa kwenye hedhi.

Katika mwaka mmoja wa masomo, hali hiyo inaweza kumaanisha kupoteza siku kati ya 30 hadi 40 za vipindi darasani, jambo linaloweza kudhoofisha ufaulu wa masomo na hata kusababisha baadhi yao kuacha shule kabisa.

Utafiti wa mwaka 2023 uliofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) unaonyesha kuwa takribani asilimia 60 ya wasichana nchini wanapata ugumu kumudu gharama za pedi mara kwa mara, hali inayofanya usafi wa hedhi kuwa changamoto kubwa kwa familia nyingi. Tatizo hilo linaonekana zaidi katika maeneo yenye changamoto za kiuchumi kama mikoa ya Tabora, Shinyanga, Simiyu, Dodoma na Kigoma, ambako kaya nyingi hupambana kukidhi mahitaji ya msingi.

Katika mazingira hayo, baadhi ya wasichana hulazimika kutumia vifaa visivyo salama kama vipande vya vitambaa au karatasi, huku wengine wakiamua kubaki nyumbani wanapokuwa kwenye hedhi ili kuepuka aibu shuleni.

Changamoto kuwa vitendo
Ni hali hiyo ndiyo iliyomsukuma Zoya kuchukua hatua.

“Baada ya kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wenzangu na kutembelea shule kadhaa, niligundua kuwa wasichana wengi hukosa vipindi kwa sababu hawana pedi au wana hofu ya kuaibika,” amesema Zoya katika mahojiano.

Ameongeza: “Niliona kuna haja ya kuwasaidia wasichana kuelewa afya ya hedhi na kuwapa msaada ili waweze kuendelea kujifunza bila hofu.”
Kupitia kampeni ya ‘Abaki Shuleni’, zaidi ya wasichana 200 kutoka shule za sekondari za Kisutu na Jangwani jijini Dar es Salaam tayari wamenufaika na elimu kuhusu usafi wa hedhi, warsha shirikishi za stadi za maisha pamoja na vifaa maalumu vilivyotengenezwa kwa ajili yao. Mpango huo pia umefanikiwa kupitia ushirikiano na mashirika kama Raising Up Friendship Foundation na Hope 4 Young Girls, ambayo yamesaidia kuendesha warsha kwa wanafunzi.

Zoya ana matumaini kuwa kampeni hiyo itapanuka na kufikia maeneo mengi zaidi nchini, ili kusaidia kukabiliana na changamoto hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi, sambamba na jitihada zinazofanywa na serikali na wadau wengine.

Wataalamu wa elimu na afya ya jamii wanasema mipango kama ya Zoya ina mchango mkubwa katika kulinda haki ya wasichana kupata elimu.

Mtafiti wa afya ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Emmanuel Msuya, anasema changamoto za hedhi bado ni moja ya sababu zilizojificha zinazochangia utoro kwa wasichana shuleni, hasa katika jamii maskini.

“Ni muhimu kuelewa kuwa hedhi si suala la afya pekee, bali pia ni suala la haki ya elimu,” amesema.

“Msichana anayekosa bidhaa za msingi za hedhi anaweza kukosa masomo mara kwa mara, na kadiri muda unavyokwenda anaweza kubaki nyuma kitaaluma na kupoteza kujiamini shuleni,” amesema.

Dk Msuya ameongeza kuwa jitihada za Zoya zinaonyesha jinsi vijana wenyewe wanavyoweza kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kijamii.

“Huu ni mfano mzuri wa uongozi wa vijana.

Taasisi za serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi zinapaswa kuunga mkono jitihada kama hizi kwa kuhakikisha pedi zinapatikana kwa urahisi shuleni,” amesema.

Kwa upande wake, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, anasema uelewa kuhusu afya ya hedhi bado ni mdogo katika jamii nyingi nchini, hali inayochangia unyanyapaa na kukosekana kwa msaada kwa wasichana.

“Wasichana wengi hupata hedhi yao ya kwanza bila kuelewa kinachoendelea katika miili yao,” ameeleza.

“Ukosefu wa taarifa na bidhaa salama za hedhi huwafanya wajisikie aibu au kulazimika kubaki nyumbani badala ya kuhudhuria masomo shuleni.”
Ameongeza kuwa jitihada za Zoya zinaonyesha kuwa hata vijana wanaweza kuleta mabadiliko yenye maana katika jamii. “Tunahitaji sera na programu zinazohakikisha kila shule inakuwa rafiki kwa wasichana, ikiwa ni pamoja na vyoo salama, maji safi na upatikanaji wa pedi,” amesema Gyumi.

Kwa Zoya, safari ndiyo inaanza.

Ndoto yake ni kuona kampeni hiyo ikiwafikia wasichana katika shule nyingi zaidi nchini Tanzania ili kuhakikisha hakuna msichana anayekosa elimu kwa sababu ya hedhi.

“Ninaamini kila msichana anastahili nafasi ya kujifunza na kufikia ndoto zake,” amesema na kuongeza:

“Ikiwa jamii itashirikiana, tunaweza kuhakikisha hakuna msichana anayeachwa nyuma.”

Kwa sasa, mpango huo unapanga kupanua shughuli zake ili kufikia shule zaidi, pamoja na kuanzisha programu za sanaa na kujenga kujiamini kwa wasichana ili kuwasaidia kutambua uwezo wao na kukuza vipaji vyao.

Katika wakati ambao familia nyingi nchini bado zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi, azma ya msichana huyo mdogo ni ukumbusho kwamba mabadiliko makubwa yanaweza kuanza kwa hatua ndogo—mradi tu kuwepo na dhamira ya kuhakikisha kila msichana anabaki shuleni.