Nyota Coastal Union kimeeleweka | Mwanaspoti

STRAIKA wa Coastal Union, Abdulkarim Segeja, amesema licha ya kuanza vibaya msimu huu, lakini kwa sasa timu imeonesha mabadiliko na mechi zilizobaki mkakati wao ni kutopoteza pointi.

Coastal Union iliyowahi kutwaa ubingwa mwaka 1988 wakati inaitwa Ligi Daraja la Kwanza kabla ya sasa kufahamika Ligi Kuu Bara, inakumbukwa pia kushuka daraja msimu wa 2015-2016 ikiwa na ndugu zao African Sports na Mgambo JKT zote za Tanga.

Msimu huu timu hiyo haijawa na matokeo mazuri baada ya kucheza mechi 16 za Ligi Kuu Bara na kushika nafasi ya 13 kwa kukusanya pointi 15, hivi sasa inajiandaa na mechi ya ugenini dhidi ya Simba, itakayochezwa Aprili 2, mwaka huu.

Katika mechi nne za nyuma, timu hiyo ya jijini Tanga imeoenakana kuwa na mabadiliko chanya ikishinda tatu ikiwano ya Kombe la Shirikisho la CDRB dhidi ya Stand United kwa mabao 4-1, huku ikipoteza moja kwa Singida Black Stars.

Segeja alisema baada ya kutoanza vyema ligi, kwa sasa matumaini yamerejea upya kufuatia matokeo waliyopata hivi karibuni, akibainisha kuwa wanajipanga na michezo inayofuata.

Alisema wakati wakiwa mapumziko mafupi, wanaendelea kutathimini mchezo ujao dhidi ya Simba pamoja na michezo mingine iliyo mbele yao akifafanua kuwa matarajio yao ni kufanya vizuri na kubaki salama Ligi Kuu.

“Tunajiandaa na mechi zijazo, hatukuwa na mwanzo mzuri ila tunashukuru kwa matokeo ya hivi karibuni tumekuwa na mabadiliko, wachezaji tumekuwa na muunganiko hali inayotupa nguvu ya kufanya vizuri,” alisema Segeja.

Nyota huyo aliongeza kwamba ligi imekuwa na ushindani kwa timu zote.