Asukile atoa matumaini mapya Prisons

PAMOJA na kukiri kuwa na matokeo yasiyoridhisha, Nahodha wa zamani wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile amesema bado ni mapema kuikatia tamaa timu hiyo, huku akiwatwisha zigo wakongwe na mastaa wa kikosi hicho kukaza kukwepa aibu ya kushuka daraja.

Asukile aliyeitumikia Prisons kwa takribani miaka 11 kisha kuvishwa gwanda la Magereza, kwa sasa anahudumu kwenye benchi la ufundi la timu hiyo huku akikumbukwa kuinusuru timu hiyo mara kadhaa kushuka daraja.

Prisons haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi mbili za chini katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi 13, leo Jumatano itakuwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma kuikaribisha Singida Black Stars kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Timu hizo zinakutana ikiwa mwenyeji Prisons imetoka kupoteza dhidi ya Yanga kwa bao 1-0, huku Singida Black Stars ikiichapa Mbeya City 4-1.

Tangu astaafu soka, Asukile amewaacha mastaa wenzake akiwamo Samson Mbangula, Jeremia Juma, Salum Kimenya, Lambart Sabiyanka na Dotto Shaban ambao wote ni askari wa Jeshi la Magereza wanaokipiga Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Asukile alisema hadi sasa ameendelea kuzungumza na wakongwe hao kuhakikisha wanaipigania nembo ya Jeshi la Magereza kwa kuwahimiza wengine kikosini ili kubaki salama Ligi Kuu Bara.

Alisema matokeo waliyonayo si mazuri japokuwa hali ya upepo mbaya si kwa Prisons pekee bali kwa timu nyingi zinahangaika, akitoa matumaini kuwa lolote linawezekana kwani hawajakata tamaa.

“Tunaye kocha mpya Shadrack Nsajigwa ambaye ameanza vizuri japokuwa amekutana na ratiba ngumu kwa kuanza na timu kubwa, tunaamini bado tunayo nafasi ya kupambana kuinusuru timu.

“Wapo wachezaji waandamizi ambao mara kadhaa tunazungumza wawahamasishe wengine kikosini kuipigania Prisons na matarajio yetu ni kufanya vizuri, wasitukatie tamaa muda upo wa kurekebisha,” alisema Asukile.

Nyota huyo aliongeza kuwa, kilio chao ni kurejea uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine jijini Mbeya kwani kucheza mechi za nyumbani kwenye viwanja vya ugenini zipo athari za moja kwa moja.

Tanzania Prisons hii itakuwa mechi ya pili mfululizo katika ligi kucheza Uwanja wa Jamhuri baada ya ule wa Sokoine kufungiwa kutokana na kukosa vigezo vya kikanuni.